Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Zao la Chikichi Mwarobaini wa Umasikini kwa Watanzania
Jan 01, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Kamishna Msaidizi wa Magereza na Mkuu wa Gereza la
Kwitanga, Dkt. Uswege Mwakahyesa akieleza namna shamba
la gereza la Kwitanga lenye ukubwa wa ekari 1,100 lililopo
mkoani Kigoma linavyoendeleza kilimo cha zao la Chikichi
nchini.

Na. Immaculate Makilika – MAELEZO

Kwa mara ya kwanza nimebahatika kuwa ziarani mkoani hapa, na
nimeshuhudia zao linalolimwa kwa wingi katika mkoa huu na nimepita
mashambani na maeneo mbalimbali na kuona miti ya kupendeza yenye
matawi mithili ya maua makubwa yenye kupendeza na kutoa matunda
mengi yenye rangi ya chungwa.

Zaidi ya hapo napata fursa ya kushuhudia ziwa la pili kwa kuwa na kina
kirefu zaidi duniani lenye samaki wa aina tofauti zaidi ya 350, na kuwa kati
ya samaki hao kuna aina ya samaki wa mapambo wanaopatikana kwa
wingi katika ziwa hilo na kuuzwa katika nchi za Ulaya na Amerika.
Chikichi ni zao linalozalisha mafuta ya mawese, mafuta ya mise, pia ni
malighafi inayotumika kuzalisha bidhaa nyingine zikiwemo sabuni, mbolea, umeme na kutazamiwa kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda nchini.

Licha ya kuwa zao hili, limelimwa kwa miaka mingi katika mkoa wa
Kigoma, bado halikuweza kuwa na tija ya kupunguza gharama za kuagiza
mafuta ya kula kutoka nje ya nchi na hasa katika nchi ya Malaysia.
Baada ya kuona fursa zilizopo katika zao la Chikichi Serikali imekua na
jitihada za makusudi za kufufua zao hili la kiuchumi nchini kwa kuanza
kushirikiana na sekta binafsi ili kuzalisha mbegu bora, kutoa elimu ya
kulima chikichi kwa wananchi na kuweka mazingira wezeshi ya wawekezaji kuja kuwekeza kwenye zao hili ikiwa ni pamoja nna viwanda vya kuchakata mafuta ya mawese.

Baada ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kuzindua Kampeni ya
Kufufua zao la Chikichi Julai 29, 2018 mnamo Desemba 19, 2020 anafanya
ziara ya siku mbili mkoani Kigoma ambapo anaiagiza Wizara ya Kilimo
kuimarisha Kituo cha Utafiti wa Zao la Chikichi kilichopo Kihinga katika
mkoa huo kwa kukitengea bajeti kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kudumu
pamoja na barabara ili kuboresha shughuli za utafiti zinazoanzwa kufanywa kituoni hapo.

Shamba la Chikichi la Gereza la Kwitanga lililopo mkoani
Kigoma ambalo linatumika kuzalisha miche ya Chikichi aina ya
Tenera ambayo baadae husambazwa katika maeneo mbalimbali
nchini.

Anasema kuwa mbegu zilizozalishwa tangu kuanza kwa zoezi la ufufuaji
wa zao la Chikichi ni 4,205,335 ambazo zinatosha kupanda eneo la ekari 84,106.7 ambapo kati yake asilimia 71 imechangiwa na Wizara ya Kilimo
kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na asilimia 29 ni
mchango wa sekta binafsi kupitia kampuni za FELISA & Ndugu
Development Foundation na Yangumacho Group.

“Hadi sasa mbegu 2,184,111 zimeshasambazwa na TARI kwa ajili ya
kuziotesha ili miche bora iweze kusambazwa kwa wakulima na kati mbegu
zinazooteshwa tayari miche 1,370,318 imeshaota na kukuzwa kwenye
viriba vidogo na vikubwa ikiwa ni hatua yua kuzifikisha kwa wakulima”
anasema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kamishna Msaidizi wa Magereza na Mkuu wa Gereza Kwitanga, Dkt.
Uswege Mwakahyesa anasema kuwa Gereza lake lina shamba lenye
ukubwa wa ekari 1,100 zilizopandwa Michikichi mwaka 1968 ambapo
lilikabidhiwa kutoka Idara ya Kilimo Mkoa wa Kigoma.

Dkt. Mwakahyesa anasema baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufika
katika Gereza hilo mwaka 2018 na kutoa maagizo kuwa liwe kituo cha
kuzalisha mbegu za Chikichiki na kusambaza maeneo mbalimbali nchini,
tayari wamegawa kwa wananchi wa vijiji vinavyozuguka Gereza jumla ya
miche 18,334 na kuwa wananchi wengi wameonesha hamasa kubwa
katika kushirki kilimo cha zao hilo.

Wakulima wa zao la Chikichi kutoka wilayani Uvinza, Kijiji cha
Itebula kitongoji cha Lugongoni B mkoani Kigoma wakichambua
miche ya Chikichi aina ya Tenera yenye sifa ya kutoa mafuta

“Mkakati wa Jeshi la Magereza ni kuhakikisha kwamba magereza yote
yenye fursa ya zao hili tutapeleka miche ili wazalishe kwasababu lengo la
jeshi letu ni kujitosheleza kwa chakula kwa hiyo hata mafuta ambayo
wanakula wafungwa magerezani yatoke kwetu wenyewe kwa kuzalisha
zaidi katika gereza hili na mengine”, anasema Dkt. Mwakahesa

Anabainnisha mikakati zaidi “Jeshi la Magereza lina shamba lenye ukubwa
wa ekari 400 huko Kimbiji, Dar es Salaam, na tayari tumeshapeleka miche
10,220 katika mkoa wa Katavi tuna shamba lenye ukubwa wa ekari 25,000
pia tumeshapeleka miche 5,220 na wataendelea kuja kuchukua miche kwa
hivyo maeneo mengi ambayo zao hili linaweza kulimwa basi tutapeleka
miche kwa ajili ya kupanda na baadae kuwapatia wananchi. Kupitia
halmshauri zao”

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Kituo cha TARI Kihinga ambaye pia
ni Mratibu wa Idara ya Usambazaji wa Teknolojia na Mahusiano, Bw. Kuzenza Lushinge anasema kuwa sasa wameanza kufanya utafiti wa zao
la Chikichi kwa kuwa ni zao linalotoa mafuta kwa wingi kuliko mazao yote
yanatoa mafuta na malengo ya Serikali ni kutatua chagamoto ya nchi
kuagiza mafuta ya kula nje ya kwa kwa asilimia 60.

“Jukumu kubwa la kufanya utafiti ni kwa ajili ya kupata mbegu bora, kwa
vile matatizo makubwa yaliyoonekana katika zao hili ni uhaba na ubora wa
mbegu kwa vile wakulima wengi wanalima kwa kwa mbegu za kienyeji
yaani Dura ambazo zinatoa mafuta kwa kiasi kidogo cha tani 1.6 kwa hekta
moja lakini Tenera inatoa tani 4 hadi 5” anasema Bw. Lushinge

Anasisitiza “kwa atakayelima kwa kutumia mbegu za kisasa aina ya Tenera
atakuwa na uzalishaji mara nne hadi tano ukilinganisha na uzalishaji wa
zamani kabla ya TARI kuanza kuzalisha mbegu za Tenera zilikua
zikiagizwa nje ya nchi kwa gharama ya dola 1 na baadae hukuzwa na
kuuzwa kwa wakulima kwa shilingi 6,000 kwa mche mmoja hii ilikua ngumu kwa wakulima kuanzisha mashamba yao ndiyo maana Serikali iliamua hiyo mbegu ya Tenera izalishwe hapa hapa nchini.”

Mchikichi uliopandwa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa
Mei 23, 2020 wenye sifa ya kutoa mafuta mengi na kukomaa
kwa muda muda mfupi katika shamba la Gereza la Kwitanga
mkoani Kigoma, ikiwa ni jitihada za Serikali za kufufua zao la
Chikichi nchini.

Hadi sasa TARI imezalisha mbegu 8,200,000 na bado inaendelea na
uzalishaji wa mbegu pamoja na kuziotesha.

Baadaa ya TARI kuzalisha mbegu hizi kwa kushirikiana na Gereza la
Kwitanga zinagaiwa katika Halmashauri ambazo zina makubaliano ya
kupanda zao hilo ambapo kimsinngi mbegu hizo hugaiwa kwa wakulima
bure.

Si hivyo tu, bali Serikali imendelea kuhimiza ushiriki wa sekta binafsi ili
kufufua zao hili la kiuchumi ambapo kumekuwepo na mazungumzo kati
yake na sekta binafsi kama ambavyo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya
FELISA and Ndugu Development Foundation, Dkt. Hamimu Hongo
anasema kuwa Tanzania inatumia fedha nyingi kuagiza mafuta ya kula nje
ya nchi ambapo zaidi ya asilimia 95 ni mafuta ya mawese ambayo ni
bidhaa ya pili kuagizwa kwa wingi baada ya mafuta ya petroli.

“Sasa mimi na timu yangu tuliona kwamba tushirikiane na Serikali tuweze
kulifufua hili zao kwa kuwa licha ya kulimwa Kigoma pia linaweza kulimwa zaidi ya mikoa kumi hapa nchini”. Anasema Dkt. Hongo

Dkt. Hongo anasema kuwa mwaka 2018 Tanzania ilitumia zaidi Dola za
Marekani milioni 300 kuagiza mafuta ya mawese kutoka nje ya nchi, likiwa
ni zao linaloweza kulimwa nchini.

“Kwa mfano mwaka 2018 mahitaji ya mafuta ya kula yalikuwa tani 50,000
kwa mwezi, kwa mwaka ni tani 600,000, lakini kuna mbegu hizi chotara
ambazo zinaitwa Tenera zina uwezo wa kutoa tani 400,000 kwa hekta
moja kwa hivyo tukiwa na wakulima 150,000 tu tunaweza kupata tani
600,000 zinazohitajika”. Anasisitiza Dkt. Hongo

Ni dhahiri kuwa jitihada za Serikali zinalenga kutatua kitendawili hiki cha
kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi kwa kuendelea kutoa mbegu bora na
elimu au utaalamu wa kutunza zao hili kwa wakulima wa mkoa wa Kigoma
na kwingineko nchini.

Kufuatia jitihada hizo za Serikali zilizoanza mwaka 2018 za kufufua zao la
Chikichi mkoani Kigoma kwa kuanzisha kituo cha utafiti ndipo Dkt. Hongo
na wenzake wakashawishika kushirikina na Serikali kuzalisha mbegu bora
kwa lengo la kusaidia kutatua changamoto ya uhaba wa mbegu ya kisasa
aina ya Tenera.

Naye, mkulima wa zao la Chikichi Bw. Fannuel Magezi kutoka Nguruka
Kijiji cha Itebula kitongoji cha Lugongoni B mkoani Kigoma anasema kuwa
aliposikia simulizi za kilimo cha kisasa alishawishika kuamua kulima zao
hilo ambapo kwa sasa ameshalima ekari 7 kati ya ekari 20 anazotarajia
kulima hapo baadae huku akiwa na matarajio ya kuwa na maisha mazuri
kama ambavyo wengi wanaeleza kuhusu faida za kiuchumi za zao la
Chikichi katika mkoa wa Kigoma.

Zao la Chikichi litakapolimwa kwa wingi nchini litatatua uhaba wa mafuta ya mawese yanayoagizwa kwa wingi kutoka nje ya nchi. Faida zingine za zao hili ni kuwepo kwa viwanda vya kuchakata mafuta ya mawese kwa ajili ya kula pamoja na viwanda vya kuchakata mafuta ya mise yanayotumika
kama ya malighafi ya kutengenezea sabuni.

Si hivyo tu bali mawese ni dawa, watu wa Afrika ya Magharibi hutumia
mafuta ya mawese kutoa sumu mwilini kama ambavyo Watanzania
wanavyotumia maziwa kumsaidia mtu aliyekunywa sumu au kemikali
hatarishi.

Halikadhalika mafuta ya mawese ni malighafi muhimu wa utengenezaji wa
vipodozi hasa lipstick au rangi ya mdomo inayopakwa na wanawake.
Hakika faida za mafuta ya mawese nyingi kama kuimarisha uoni, kuondoa
makunyazi katika ngozi huku yakitajwa kuwa mafuta yenye bei nafuu zaidi
kuliko mafuta ya yoyote yale duniani.

Utakubaliana nami kuwa zao hili ambalo ni rahisi kutunza baada ya
kupanda na lenye kudumu kwa zaidi ya miaka 200 h huku mkulima
akiendelea kuvuna kwa miaka kati ya 30 hadi 40 huku likimhakikishia
mkulima kipato cha muda mrefu huenda ndio zao linaloweza kubadilisha
maisha ya Watanzania kwa kukuza vipato vyao na kufikia uchumi wa juu.

Halikadhalika, upatikanaji wake wa soko hapa nchini na katika nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) ni dalili tosha kuwa Chikichi ni mwarobaini wa umasikini kwa
Watanzania.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi