Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mhe. Suleiman Masoud Makame amesema uzalishaji wa matango bahari na uboreshwaji wa zao la mwani una manufaa makubwa kwa Zanzibar na nchi za pembezoni mwa ukanda wa Bahari ya Hindi.
Waziri Suleiman Masoud Makame, ameyasema hayo wakati akifungua semina ya siku 5 kuhusu namna bora ya uzalishaji wa vifaranga vya matango bahari na ukulima bora wa zao la mwani iliyofanyika katika Hoteli ya Verde mjini Zanzibar jana tarehe 07 Novemba, 2022.
Mhe. Suleiman ameongeza kuwa, kufanyika kwa Mkutano huo mjini hapo kutaleta mafanikio kwa kuwa wajumbe watapata nafasi ya kujadiliana juu ya namna bora ya kuzalisha mazao ya baharini ikiwemo vifaranga vya matango bahari.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Dkt. Aboud Suleiman Jumbe amesema mkutano huo wa wataalamu kutoka katika nchi za IORA utafungua milango kwa watalamu na kuona namna gani Zanzibar ilivyojiandaa katika uchumi wa buluu na uvuvi.
"Nchi za ukanda wa pembezoni mwa bahari ya hindi watajifunza mambo mengi hapa Zanzubar kwa vile kuna wizara ya uchumi wa buluu na uvuvi", ameeleza
Nae Mkurugenzi wa Uchumi wa Buluu, Bi. Rina Setyawati kutoka ukanda wa Bahari ya Hindi Nchi za IORA zimekuwa na ushirikiano wa pamoja katika mambo mbalimbali ikiwemo katika suala zima la kujifunza ubora wa kuzalisha vifaranga vya matango bahari na kilimo bora chenye faida kwa nchi wanachama.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mratibu wa Masuala ya Jumuiya ya Nchi za Mwambao mwa Bahari ya Hindi (IORA), Balozi Agnes Richard Kayola akizungumza katika Mkutano huo ameeleza kuwa IROA ina imani kuwa Mkutano huo utakuwa na tija kubwa kwa wanachama waliotoka nje ya Tanzania kwa vile watapata muda wa kubadilishana uzoefu jinsi ya kufanikiwa katika kilimo cha mwani kwa wananchi.
Aidha, katika kipindi cha siku 5 cha semina hiyo wakulima wa mazao mbalimbali ya bahari watapata fursa ya kuonesha bidhaa zao sambamba na utaalam wanaoutumia kuzalisha mazao hayo. Hatua hiyo itawapa wakulima hao nafasi ya kujifunza zaidi kuhusu uchumi wa buluu, sambamba na kujipatia fursa za makoso mapya ya mazao yao.