Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Zaidi ya Wananchi Milioni Moja Kunufaika na Mradi wa Maji Arusha
Sep 12, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Beatrice Lyimo – MAELEZO, Arusha

Zaidi ya wananchi milioni moja kunufaika na Mradi wa Kuboresha Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA).

Hayo yameelezwa na mratibu wa mradi huo Mhandisi Gasto Mkawe wakati akiwasilisha taarifa fupi ya mradi wakati wa ziara ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa alipotembelea ofisi za mamlaka hiyo na hatimae kutembelea baadhi ya mitambo ya kutibu maji, matanki ya maji pamoja na miradi mbalimbali inayotekelezwa jijini Arusha.

Mhandisi Mkawe amesema kuwa lengo la mradi huo ni kuboresha hali ya upatikanaji wa majisafi na kuboresha huduma ya uondoaji wa majitaka katika Jiji la Arusha ili kuboresha afya na hali ya maisha ya wakazi wa jiji kwa ujumla wake.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imewekeza katika kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika Jiji la Arusha ili kuondoa kero ya upungufu wa majisafi na uondoaji majitaka katika Jiji la Arusha na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Arumeru ili kuendana na kasi ya ukuaji wa Jiji la Arusha” ameeleza Mhandisi Mkawe.

Ameongeza kuwa “Mradi utaongeza uzalishaji wa maji kutoka wastani wa lita 40,000,000 kwa siku hadi kufikia lita 200,000,000 kwa siku na kutosheleza zaidi ya asilimia 100 ya mahitaji ambayo kwa sasa ni lita 109,689,250 kwa siku, mradi utaongeza idadi ya wakazi wanaopata majisafi kutoka wastani wa watu 325,000 hadi kufikia watu 600,000 wakiwemo wastani wa watu 250,000 wanaoingia na kutoka jijini kila siku, wananchi 159,348 kutoka Wilaya ya Arumeru, Hai na Mkoani Kilimanjaro na kutoka Simanjiro mkoani Manyara ambao wanapitiwa na miundombinu ya mradi” amefafanua Mhandisi Mkawe.

Aidha, hadi kufikia julai, 2022 mradi huo umekamilika kwa asilimia 93% ambapo mikataba 10 imeshakamilika huku mikataba mitano iko katika hatua mbalimbali ya utekelezaji, mradi huo ulianza kutekelezwa februari 2016 na unatarajiwa kukamilika Juni, 2023.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa yupo Jijini Arusha kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan..

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi