Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Zaidi ya Bilioni 98 Kupeleka Umeme Gridi Imara Kilindi
Jan 08, 2024
Zaidi ya Bilioni 98 Kupeleka Umeme Gridi Imara Kilindi
Meneja TANESCO Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Mha. Edward Mwakapuja akizungumza kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Gridi Imara wilayani humo.
Na Mwandishi Wetu

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya bilioni 98 katika Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Gridi imara ili kutatua changamoto ya umeme wa uhakika katika wilaya hiyo.

Hayo yameelezwa na Meneja TANESCO Wilaya ya Kilindi,  Mha. Edward Mwakapuja na kusema kuwa Wilaya hiyo imekuwa na changamoto kadhaa ya kutokuwa na umeme wa uhakika kwa sababu mbalimbali.

“Laini zinazoleta umeme Kilindi ni za ukubwa wa kati wa voti 33,000 ambapo line hizo zinatoka pande mbili tofauti, moja kutokea kituo cha Kondoa laini hiyo imepita wilaya za chemba, kuna michepuko kwenda sehemu za wilaya ya kongwa na chamwino na inapitia wilaya ya Kiteto ndipo inafika Kilindi ambapo inaurefu wa kilometa 220”

“Upande mwingine ni kutokea vituo vya Hale au Kasiga kupitia Wilaya za Korogwe, Handeni kisha kufika Kilindi umbali wake ni zaidi ya kilometa 250, kutokana na urefu huo ambapo laini zinapita kuna transforma kadhaa kulisha maeneo hayo ambapo imepelekea kama kuna hitilafu yoyote njiani au kuna matengenezo katika wilaya tunazopakana nazo moja kwa moja Wilaya ya Kilindi inaathirika,” ameeleza Mha.Mwakapuja.

Aidha amesema kuwa, changamoto hizo zimepelekea Serikali ya Awamu ya Sita kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambapo utahusisha ujenzi wa laini ya voti 132,000 kutoka Mkata yenye urefu wa Kilometa 143 na ujenzi wa kituo kikubwa cha umeme kitakachopokea umeme wa voti 132,000 na kuupoza kuifikia voti 33,000 ili kusambazwa wilaya ya kilindi na kupeleka wilaya jirani.

Akizungumza faida za mradi huo Mha. Mwakapuja amebainisha kuwa, wilaya ya kilindi utakuwa na umeme wa uhakika kutoshereza ongezeko la umeme hasa kwa miradi inayotarajiwa kuongezeka ya uchimbaji madini, lakini pia ukatikaji wa umeme utapungua kwani laini itakayopeleka umeme wa voti 132,000 utapita moja kwa moja bila ya kuwa na matumizi njiani.

Mbali na hayo, Bw. Yusuph Ahmad ameishukuru Serikali kwa jitihada za kupeleka mradi wa umeme wa gridi imara wilayani humo ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi na kusaidia kukuza shughuli za kiuchumi na maendeleo kijamii.

Utekelezaji wa mradi huo ulianza rasmi mwezi Juni, 2023 katika eneo la Kitongoji cha Mnazi Kijiji cha Kwamwande na unatarajiwa kukamilika mnamo mwezi Desemba, 2024.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi