Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wizara Yaombwa Kutoa Tuzo kwa Wanahabari Wanaotetea Watoto.
Nov 20, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_23040" align="aligncenter" width="583"] Mwanafunzi wa Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Steven Mkomwa akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati alipokuwa akizindua makala yake ya ‘habari na mtoto’ kuelekea katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto Duniani yanayofanyika Novemba 20 ya kila mwaka. Mkutano huo umefanyika leo Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO.[/caption]

Na Jacquiline Mrisho.

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,  Wazee na Watoto imetakiwa kutoa motisha na kutoa tuzo maalum kwa waandishi wa habari wanaoandika habari,  makala na kuandaa vipindi vya kuelimisha jamii kuhusu haki na utetezi wa watoto.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mwanafunzi wa Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Steven Mkomwa wakati alipokuwa akizindua makala yake ya ‘habari na mtoto’ kuelekea katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto Duniani yanayofanyika Novemba 20 ya kila mwaka.

Mkomwa alisema kuwa ufinyu wa ushirikiano kati ya vyombo vya habari na Asasi za Kiraia au Wizara yenye dhamana ya watoto ni moja ya kikwazo katika suala zima la utetezi wa mtoto hivyo ni vyema kuboresha na kuyadumisha maudhui haswa pale wadau wanapoonesha utayari wao katika kupigania ustawi wa watoto nchini.

“Sisi kama Taifa kupitia Wizara yenye dhamana ya watoto iko haja ya kutambua michango ya wanahabari wanaokwenda maili za ziada katika kuripoti na kumtetea mtoto kwa kutoa tuzo za motisha na utambuzi ili kutengeneza na kuchochea mazingira ya habari za kina na zenye uhalisia”, alisema Mkomwa.

Mkomwa ameongeza kuwa ili kuchochea mchakato wa utoaji wa tuzo hizo, amedhamiria kuandika barua ya wazi kwa Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya watoto kwa kujenga hoja na kushawishi ni kwa namna gani mchakato huo unavyoweza kufanyika kwa kushirikisha wadau wa haki za watoto na huduma kwa watoto.

Akifafanua zaidi, Mkomwa alisema kuwa kuwa tuzo hizo zinaweza kufanyika kila mwaka kwa kutambua michango ya vyombo vya habari kupitia waandishi wa habari wenye jitihada za kuandika habari za kutetea watoto, wahariri, wamiliki au wasimamizi wa vyombo husika vya habari pamoja na wadau wengine nje ya tasnia ya habari.

Aidha aliiomba wizara hiyo pamoja na wananchi kujifunza kutokana na matokeo yaliyotolewa katika utafiti uliofanywa na shirika la Internews Europe mnamo mwaka 2013 ambao uligundua kuwa kuna ufinyu wa sauti za watoto katika mikondo ya Vyombo Vikuu vya Habari kuandaaa viwango, taratibu na miongozo ya kitaaluma katika kuripoti habari dhidi ya haki kwa mtoto.

Tarehe 20 Novemba ya kila mwaka, Dunia inaadhimisha Siku ya Mtoto Duniani ambayo ni mahsusi katika kuonesha umuhimu wa ulinzi na utetezi kwa mtoto pamoja na kufanya tathmini za kikanda na kidunia juu ya viwango vya ukiukwaji na ukatili wa haki za watoto.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi