Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wizara Yakamilisha Mwongozo wa Maadili ya Taifa na Utamaduni wa Mtanzania
Aug 18, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na John Mapepele, WHUSM

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo ni msimamizi na mratibu wa shughuli zote zinazohusu maendeleo ya utamaduni nchini, leo Agosti 18, 2021 imefanya kikao na wadau mbalimbali nchini ili kutoa maoni ya Mwongozo wa Maadili ya Taifa na Utamaduni wa Mtanzania katika ukumbi wa Wizara eneo la Mtumba jijini Dodoma.

Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni, Dkt. Emmanuel Temu, ametanabaisha kuwa lengo la kikao hicho ni kuboresha Mwongozo wa Maadili ya Taifa na Utamaduni wa Mtanzania ili kulinusuru Taifa dhidi ya mmomonyoko wa Maadili na utamaduni wa nchi yetu kwa ujumla wake.

“Kitabu kinalenga kutoa mwongozo kwa jamii ya kitanzania kurejea katika misingi yetu ya maadili kama Taifa kwa kupenda, kuthamini na kuheshimu mila na desturi zetu ambazo ni miongoni mwa nguzo kuu za utamaduni wetu”,amefafanua Dkt. Temu.

Aidha, amesema kitabu hicho cha Mwongozo kinazingatia tamko la Sera ya Utamaduni la mwaka 1997, Sura ya Pili, Kipengele cha Pili, Sehemu ya Tatu (2:2:3) kuwa tuna wajibu wa kurithisha na kuendeleza Maadili, Mila, na Desturi nzuri.

Pia, Kitabu hicho kinakusudia kutoa mwelekeo na umuhimu wa kuzingatia maadili kwa makundi mbalimbali ya jamii wakimemo wanafunzi katika ngazi mbalimbali za elimu, vijana, watumishi wa umma na jamii kwa ujumla.

Akiwapitisha wajumbe katika yaliyomo ya kitabu hicho, Mkurugenzi Msaidizi wa Utamaduni anayeshughulikia eneo la Lugha, Dkt. Resan Mnata amesema kitabu hicho kina jumla ya sura tano, ambapo sura ya Kwanza imejikita katika Usuli; Sura ya Pili mmomonyoko wa maadili katika jamii; Sura tatu wajibu wa makundi mbali mbali katika kukuza na kuendeleza Utamaduni na maadili; Sura ya nne Usimamizi, uhifadhi, utekelezaji na uendelezaji wa utamaduni na maadili na Sura ya tano mambo muhimu ya kuzingatia na mapendekezo.

Akichangia katika kikao hicho, Mjumbe kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bi. Bona Leon ameshauri baada ya kukamilika kwa muongozo ni muhimu kukatengenezwa kitabu kidogo chenye lugha rahisi kitakachosambazwa kwa jamii ili ujumbe uliokusudiwa uweza kuwafikia watu wengi kwa urahisi.

Katibu Mkuu wa Habari, Dkt. Hassan Abbasi katika Dibaji amesema kitabu hiki kinaeleza juhudi za Serikali za kukuza na kujenga Maadili na Utamaduni wa Mtanzania ambapo amefafanua kwamba uhai na utambulisho wa Taifa lolote duniani, hutegemea utamaduni wa Taifa husika.

“Kwa maneno mengine, utamaduni ni kielelezo na utambulisho wa Taifa na watu wake”, Amehitimisha Dkt. Abbasi

Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Innocent Bashungwa kwenye kurasa wake wa ujumbe wa Mhe Waziri amesema anaamini  Kitabu hicho cha Muongozo kitatumika kama nyenzo muhimu katika kulirejesha Taifa kwenye misingi ya maadili ya taifa na utamaduni wa  mtanzania na  kuwa kitasaidia kulinusuru Taifa la Tanzania kutoka katika minyororo ya tamaduni za kigeni na kujenga moyo wa kuthamini, kudumisha na kuendeleza Maadili mema kwa Jamii ya Watanzania wote.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi