Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wizara ya Michezo Yapongezwa Kuwa na Michezo ya Kipaumbele
Aug 21, 2023
Wizara ya Michezo Yapongezwa Kuwa na Michezo ya Kipaumbele
Kamati ya Bunge ya Elimu, Michezo na Utamaduni chini ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mussa Sima wakisikiliza taarifa iliyowasilishwa leo Agosti 21, 2023 jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Saidi Yakubu kwa niaba ya Waziri Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana
Na Na Mwandishi Wetu

Kamati ya Bunge ya Elimu, Michezo na Utamaduni chini ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Mussa Sima imepokea na kujadili taarifa ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhusu michezo ya kipaumbele ambapo wamepongeza kwa hatua hiyo ambayo itatangaza vyema nchi, huku wakisisitiza idadi ya michezo hiyo kuwa ndogo inayoweza kusimamiwa vyema.

Katika taarifa hiyo iliyowasilishwa leo Agosti 21, 2023  jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Saidi Yakubu kwa niaba ya Waziri Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana amesema Serikali imeamua kuwa na michezo ya kipaumbele ili kufanya vizuri kimataifa.

"Tumeamua kuwa na michezo sita ya kipaumbele ambayo ni  Mpira wa Miguu, Netiboli, Kikapu, Wavu, Riadha na Ngumi ambayo Serikali kwa kushirikiana na wadau itadhamini michezo hiyo,” amesema Katibu Mkuu, Bw. Saidi Yakubu.

Amesema katika michezo hiyo, tayari mafanikio yameanza kuonekana ikiwemo ushiriki wa michezo ya CHAN nchini Cameroon,  Twiga Stars kushiriki COSAFA nchini Afrika Kusini, Timu ya Fountain Gate kutwaa Kombe la Shule za Sekondari Afrika, Tanzania kuwa mwenyeji wa  sekretarieti ya Michezo Kanda ya Nne Afrika pamoja na kushirikiana na Kenya na Uganda kuwa mwenyeji wa AFCON mwaka 2027, pamoja na Mabondia Hassan Mwakinyo, Twaha Kiduku, Fatma Yazidu na Karim Mandonga.

Akijibu hoja mbalimbali za Wajumbe wa Kamati hiyo, Waziri  Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema wizara inaendelea kuboresha miundombinu ya michezo, kwa kushirikiana na Ubalozi wa India hapa  nchini itawezesha kupatikana kwa Kocha wa mchezo wa Kabadi na Ubalozi wa Ufaransa hapa nchini utadhamini wanamichezo chini ya miaka 17 kujifunza mpira nchini Ufaransa.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti, Mhe. Mussa  Sima amesema kamati itafuatilia suala la asilimia tano ya Mchezo wa Kubahatisha namna inavyochangia katika Mfuko wa Michezo ikiwemo upatikanaji na kiasi kinachopatikana kwa wakati gani, huku akisisitiza suala la michezo ya vipaumbele  kuwa michache.

Kwa upande wa Wajumbe wa Kamati hiyo wakati wanachangia taarifa hiyo, wameishauri wizara kuwa na michezo michache ili iweze kuisimamia na kuiendesha vizuri.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi