Wizara ya Maliasili na Utalii imeibuka mshindi namba moja kwenye mbio za mita 3,000 na mita 800 na kutinga fainali kwenye mbio za mita 400 huku ikiingia nusu fainali kwenye mbio za mita 200 katika mashindano ya 37 ya Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayoendelea mkoani Iringa.
Akizungumza leo mkoani humo mara baada ya ushindi, Bw. Elibariki Buko ambaye ndio mshindi namba moja wa mbio hizo za mita 3000 na mita 800 na pia ndiye amefanikiwa kuipatia ushindi Wizara kwa kuingia fainali ya mita 400 pamoja na nusu fainali ya mita 200, amesema ushindi huo utasaidia kuimarisha michezo na kuutangaza utalii nchini.
"Ushindi huu ni muhimu sana kwetu, tunaushukuru uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuhamasisha michezo, ushindi huu ni moja ya sehemu ya kusaidia juhudi za kutangaza utalii kupitia filamu ya The Royal Tour ya Rais wetu mpendwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan." amesema Buko.
Naye Mwenyekiti wa Timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Getrude Kassara amesema Wizara itahakikisha inaendelea kupambana ili kushinda michezo iliyobakia na hatimaye kubeba vikombe vyote.
" Tumefurahi tumeshinda riadha, lakini si riadha tu, tumekuja kupambana katika michezo mingine pia lengo letu likiwa ni kutangaza utalii kupitia michezo. Amesema Getrude
Jumla ya michezo 10 imechezwa, kwa upande wa wanaume ambapo mbio za mita 3000 na 800, Bw. Elibariki Buko ameibuka mshindi huku akiingia fainali kwenye mbio za mita 400 na nusu fainali kwenye mbio za mita 200 na mita 100 Bw. Didace Dawson akiwa ameshika nafasi ya 5.
Aidha, kwa upande wa wanawake, Bi. Jehovaness Sarakikya ameshika nafasi ya 4 kwenye mbio za mita 3000 na mbio za mita 800 na katika mashindano ya urushaji Tufe mwanamichezo, Jumanne Ally na Twitike Sengerema wote walifanikiwa kushika nafasi ya 5.
Kwa upande wa mchezo wa kamba, Timu ya Wanawake hapo kesho itamenyana vikali na Timu ya Hazina katika hatua ya mtoano ya raundi ya kumi na sita bora (Round 16) huku mwanariadha Elibariki Buko akishindana katika mchezo wa riadha kwenye hatua ya nusu fainali mbio za mita 200, fainali katika mbio za mita 400 na pia katika mashindano ya mbio za mita 1,500.