Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amewataka Watendaji wa Wizara na Taasisi kujipanga kimkakati kwa kubuni miradi yenye tija kwenye Sekta ya Madini itakayowezesha kuongeza Bajeti ya Wizara na kuhakikisha inakwenda sambamba na Vipaumbele vya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, Dira ya 2030 Madini ni Maisha na Utajiri pamoja na Vipaumbele vya Taifa.
Ametoa rai hiyo leo Oktoba 6, 2023, wakati wa kikao na baadhi ya Watendaji wa Wizara na Wakuu wa Taasisi za Wizara, ambacho pia kimehusisha watendaji wanaohusika na masuala ya Mipango, Fedha na Rasilimaliwatu kilicholenga kujadili na kujipanga kutekeleza maelekezo, vipaumbele vya wizara, majukumu, mipango na program mbalimbali ambazo zilijadiliwa wakati wa vikao vya Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde alivyofanya na taasisi zote chini ya Wizara baada ya kuteuliwa na kuapishwa kuwa Waziri wa Madini kwa lengo la kufahamiana, kujengeana uelewa na kuweka mikakati ili kuongeza tija kwenye Sekta ya Madini
Aidha, katika kikao hicho, watendaji hao wamepata wasaa wa kufahamishwa kuhusu namna ya kuandaa mipango na miradi ya kisekta yenye tija kwa taifa kwa kuhakikisha inakwenda sambamba na vipaumbele vilivyopangwa na wizara na vile vya kitaifa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mchumi Mwandamizi kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, Khalid Shekimweli amesisitiza kuwa miradi na mipango inayopangwa na sekta ni vema ikazingatia maeneo makuu ya msingi ambayo ni pamoja na kuzingatia masuala yanayohusu huduma muhimu za kijamii, yanayokusudia kuondoa umaskini pamoja na kukuza uchumi.
Awali, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini, Bw. Augustino Olal ameeleza kuwa katika Mwaka wa Fedha wizara imepangiwa bajeti ya Shilingi Bilioni 89.3 ambayo imelenga kutekeleza vipaumbele Sita vya Wizara.
Amevitaja vipeumbele hivyo kuwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli, kuongeza Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa, kuendeleza Madini Muhimu na Madini Mkakati, Kuwaendeleza na kusogeza Huduma za Ugani kwa Wachimbaji wadogo, kuhamasisha shughuli za Uongezaji thamani Madini na kuhamasisha uwekezaji na Biashara katika sekta ya Madini na Uanzishwaji wa Minada na Maoneshi ya Madini ya Vito.