Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wizara ya Afya Yajidhatiti Mpaka wa Rusumo Kukabiliana na Ebola
Oct 13, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Faustine Gimu Galafoni - Kagera.

Katika kuhakikisha maeneo mbalimbali ya mipakani yanakuwa salama dhidi ya magonjwa ya mlipuko kutoenea zaidi kutoka nchi moja hadi nyingine, Wizara ya Afya imejidhatiti kwa kuweka sheria na taratbu mbalimbali za afya kwa maeneo ya mipaka na yenye mwingiliano mkubwa wa watu ikiwemo kituo cha utoaji wa huduma kwa pamoja Rusumo mkoani Kagera kinachounganisha nchi ya Tanzania na Rwanda.

Akizungumza na Waandishi wa Habari  mara baada ya kutembelea katika mpaka huo, Afisa Afya Mfawidhi kutoka Mpaka wa Rusumo,  Oswad Kimasi amesema  katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Ebola, hatua ya kwanza kwa abiria wote wanaofika mpaka  wa Rusumo ni kunawa mikono kwa maji tiririka na taratibu zingine kufuatwa ikiwemo kupimwa joto na kupatiwa vipeperushi vyenye ujumbe kuhusu masuala ya afya.

“Abiria anapofika hapa kwanza kabisa ananawa mikono kwa maji tiririka na hatua zinazofuata ni vipimo kisha tunatoa vipeperushi pamoja na elimu ya afya kwa wasafiri wote wanaoingia katika mpaka huu,” amesema.

Kwa upande wake Meneja wa Mpaka huo, kituo cha utoaji wa huduma kwa pamoja Rusumo ambaye pia ni  Afisa kutoka mamlaka ya mapato Tanzania[TRA]kituoni hapo   Mohammed Mnonda amesema  kitengo cha afya kituo cha utoaji wa huduma kwa pamoja Rusumo kimepewa majukumu ya kuratibu shughuli zote zinazohusu afya ikiwemo kupima abiria na wajibu wa kutoa elimu juu ya magonjwa mbalimbali ya mlipuko .

“Katika mpaka wetu kila idara inawajibika mfano kuhusu suala la upimaji wa abiria kitengo cha afya kinahusika kituoni hapa  kuhakikisha kila abiria anapimwa “amesema.

Naye mmoja wa abiria aliyekuwa anapita katika mpaka huo kati ya Tanzania na Rwanda Semakura Athuman amesema amekuwa na uelewa mkubwa kuhusu ugonjwa  wa Ebola kutokana na serikali kupitia Wizara ya Afya ,Idara ya Kinga ,Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma kuweka mkazo mkubwa wa utoaji wa elimu kila kona ya Tanzania.

“Kuhusiana na Ebola hii,mwanzoni nilikuwa sielewi lakini sasa najua dalili zake,mfano kutapika ,kutokwa damu,na pia nimejua sasa unaweza kuenezwa kwa kula wanyamapori kama vile nyani,na  mara tu ya kufika hapa nimeona vipeperushi ,nikapatiwa elimu ya afya”amesema Athuman.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi