Baada ya miaka minne ya kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19, Wizara ya Afya imechukua jukumu la kufanya zoezi la tathmini kwa namna ilivyokabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo nchini.
Hayo yamesemwa leo na Mfamasia Mkuu wa Serikali, Bw. Daudi Msasi wakati akifungua kikao cha kwanza kwa zoezi hilo la tathmini kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.
“Wizara imeona ni wakati sahihi kufanya tathmini hiyo na kwa mujibu wa kanuni za udhibiti wa magonjwa ya mlipuko, ni vizuri kufanya tathmini ili kuimarisha namna ya kukabiliana na magonjwa kama hayo kwa nyakati za usoni,” amesema Bw. Msasi.
Amesema, lengo ni kuainisha masuala yaliyofanyika vizuri, kubaini changamoto na mapungufu katika mapambano ya UVIKO-19, na namna ya kuweza kukabiliana na matukio kama hayo endapo yatajitokeza kwa nyakati zijazo.
Aidha, Bw. Msasi amewataka washiriki wote kwenye kikao hicho cha tathmini kuwa huru katika kutoa taarifa sahihi na maoni yao kwa kuwa kikao hicho hakina lengo la kumlaumu yeyote wala kunyosheana vidole bali kimelenga zaidi kufanya tathmini na kuboresha njia nzuri zaidi za kuweza kukabiliana na majanga kama ya UVIKO-19 endapo yatajitokeza tena nchini.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa Wizara ya Afya, Dkt. Angela Samwel amesema tathmini hiyo baada ya kukabiliana na mlipuko wa UVIKO-19 imehusisha wadau mbalimbali kutoka Wizara, Taasisi za Serikali, Waganga Wakuu wa Mikoa, Hospital za Serikali na Binafsi na wengine kutoka Mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wa maendeleo.
Dkt. Angela amesema taarifa ya tathmini hiyo itahusisha masuala mazuri yaliyofanyika wakati wa kukabiliana na UVIKO-19, Changamoto na Mapungufu pia itapendekeza hatua za muda mfupi na muda mrefu za kuchukua ili kuendeleza masuala mazuri na kuboresha mapungufu yaliyojitokeza, ambapo itawasilishwa kwa viongozi na wadau mbalimbali