Kamati ya Kitaifa ya kuendeleza michezo nchini inayojumuisha Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo, Baraza la Michezo la Majeshi Tanzania (BAMMATA), Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) leo Oktoba 12, 2021 jijini Dar es Salaam wamepitisha mpango wa muda mfupi wa kuandaa Timu za Michezo za Taifa zitakazoshiriki Michezo ya Jumuiya ya madola nchini Uingereza mapema Julai hadi Agosti 2022.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Nasra Mohamed amesema tayari kamati yake imepitisha mpango huo hatua inayofuata ni kupeleka kwa Wizara yenye Sera na dhamana ya michezo nchini ili utekelezaji wake uanze mara moja kulingana na ratiba.
“Ninafuraha kusema kuwa mpango huu umeandaliwa vizuri sana na wataalam wa michezo ni matumaini yetu kabla ya mwezi ujao utakuwa umewasilishwa Wizarani ili tupate baraka na maelekezo yatakayosaidia utekelezaji wake”. Amefafanua Afande Mohamed
Aidha, amesema Kamati imeteua Kamati ndogo ambayo itafanya kazi ya kuainisha mpango unaonyesha timu zitakazoshiriki, vifaa vya michezo, aina ya michezo itakayochezwa, wachezaji wa kila mchezo na kambi kwa ajili ya michezo hiyo ambapo amesema kambi hizo zitatakiwa kuanza rasmi mapema Januari 2022.
“Tumeitaka kamati ndogo kufanya kazi usiku na mchana na kukutana na wataalam wa michezo, mashirikisho na vyama vya michezo kwa kuwa kila mchezo una taratibu zake ”. Amesisitiza Afande Nasra
Naye, Mwenyekiti Mwenza wa kamati hiyo, Addo Komba ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo kutoka Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Michezo amesema uundwaji wa kamati hiyo ya kitaifa utasaidia kuleta mageuzi makubwa na hatimaye ushindi kwenye mashindano ya kimataifa yatakayoanza mwakani.
“Kipekee namshukuru Mhe. Rais kwa maelekezo yake ya kutaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na Wizara tukae na kuaundaa Kamati kwa ajili ya kuboresha michezo nchini ambapo leo tumeshuhudia Mpango wa Muda mfupi wa kuandaa Timu za Taifa umekamilika”. Amefafanua Mkurugenzi Komba
Kaimu Katibu wa BMT Neema Msitha amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na kamati ndogo na kutaka bajeti na gharama halisi kwa ajili ya mashindano hayo iandaliwe ambapo amesema ikikamilika italisaidia taifa kupiga hatua kwenye michezo kama ilivyokuwa kwenye siku za nyuma.