Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Serikali mbalimbali na Taasisi za haki za binadamu kuendelea kuchukua hatua za kuimarisha ulinzi na utetezi wa haki za binadamu na kushughulikia kikamilifu changamoto zilizopo.
Dkt. Mwinyi ametoa wito huo leo Oktoba 20,2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kilichopo jijini humo wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.
“Ni vyema ikakumbukwa kuwa kila mwaka ifikapo tarehe 21, Oktoba, Bara la Afrika linaadhimisha Siku ya Haki za Binadamu Afrika ambapo Kaulimbiu ya mwaka huu wa 2023 ni “Kuimarisha na Kuendeleza Utamaduni wa Haki za Binadamu kwa Nyakati zijazo’’, amebainisha Dkt. Mwinyi.
Aidha, ameongeza kuwa, kaulimbiu ya siku ya haki za binadamu ya Afrika ya mwaka huu, inashawishi kukumbusha wadau kutoka Taasisi za Kitaifa za Haki za Binadamu, AZAKI na wadau wengine wote kuwa haki za binadamu tunazotetewa ziendane na kauli mbiu hiyo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza na kusimamia haki za binadamu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo.
“Katika katiba yetu, haki za binadamu zimeainishwa kuanzia Ibara ya 12 hadi 24 lakini pia Katiba yetu kuanzia Ibara ya 25 hadi 30 imeainisha wajibu wa kila raia. Katika kuhakikisha tunazilinda haki za binadamu na watu, hapa Tanzania tulianzisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Taasisi hii ya kitaifa, tumeianzisha kwa lengo la kutetea, kulinda na kuhifadhi haki za binadamu nchini” ameongeza Rais Mwinyi.
Vilevile “jitihada mbalimbali zimechukuliwa na Serikali ili kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na kutekelezwa kwa mujibu wa Mikataba ambayo Tanzania ni mwanachama; Kwa kiasi kikubwa, jitihada hizi zimeboresha hali ya upatikanaji wa haki mbalimbali ikiwemo haki ya usawa mbele ya sheria, afya, elimu, maji na mazingira safi, uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa kuabudu, ajira, haki ya kumiliki mali na uhuru wa vyombo vya habari”.
Akizungumza kuhusu uhuru huo, Rais Mwinyi amebainisha kuwa, kwa sasa Tanzania ina vyombo vingi vya habari vikiwemo redio 210, televisheni 56, magazeti 288 pamoja na mitandao mbalimbali ya kijamii na kufikia hatua ya kuimarika kwa uhuru wa kidemokrasia, haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.
Kikao cha 77 cha Kawaida cha Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu hapa nchini kinafanyika Jijini Arusha ambapo katika siku 11 kutakuwa na vikao vya washiriki wote (public session) na siku 9 za vikao vya Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (private session).