Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kagera Waishukuru Serikali ya Marekani kwa Kufadhili Mafunzo ya WISN+POA kwa Watumishi wa Sekta ya Afya.
Jun 07, 2018
Na Msemaji Mkuu

 Na: Nashon Kennedy- Kagera

MKOA wa Kagera umeuishukuru Serikali ya Marekani kupitia Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo za Sekta za Umma (PS3) kwa ufadhili wake wa mafunzo ya ujengaji uwezo wa mifumo ya utendaji kazi na fedha serikalini ambayo  imekuwa ikiyatoa kwa watumishi wa kada mbalimbali hapa nchini.

Pongezi hizo zimetolewa jana mjini Bukoba na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Diwani Athuman alipokuwa akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili ya matumizi ya utaratibu wa upangaji wa watumishi kwa kutumia Mfumo unaozingatia uzito wa kazi kwa halmashauri maarufu kama (WISN+POA) utakaoimarisha huduma za afya na takwimu za watumishi.

“ Niwashukuru PS3 kwa kuwezesha mipango hii ya utoaji wa mafunzo haya kufanyika kwa watumishi wetu hawa, hili ni jambo kubwa kwa maendeleo ya nchi yetu”, alisema na kuishukuru Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa kwa kutoa raslimali watu katika kuwezesha mafunzo hayo ya siku mbili yanayohudhuriwa na Makatibu Tawala wasaidizi, watumishi wa afya na utumishi kutoka mikoa ya Geita na Tabora.

Aliwataka watumishi waliohudhuria kwenye mafunzo hayo kuhakikisha kuwa wanatoa muda mwingi wa ushiriki ili waweze kupata uelewa mkubwa iutakaowawezesha kutekeleza vyema majukumu yao katika halmashauri na mikoa yao.

“ Kama ni suala la kui-push nchi iende mbele ni sisi hawa tulioko humu ndani tuna wajibu huo, hivyo kila mtu ahakikishe kuwa anakwenda kutimiza wajibu wake ipasavyo baada ya mafunzo haya”, alisisitiza.

Aidha, alisema baada ya mafunzo hayo, viongozi na watumishi hao wa umma wataondoa visingizio lukuki kutoka maeneo yao ya utendaji, ikiwemo kutotumika kwa baadhi ya mifumo iliyo kwenye halmashauri yao, ambapo aliwakumbusha umuhimu wa kuitumia mifumo hiyo kikamilifu kwenye ukusanyaji wa mapato kwenye halmashauri zao.

Aliwataka watumishi kutumia kikamilifu mifumo mbalimbali iliyopo kwenye maeneo yao ili iweze kuleta ufanisi na malengo yaliyokusudiwa, akionya kuwa moja ya changamoto iliyokuwepo kwa muda mrefu ni aina nyingi ya mifumo ambayo imekuwa ikitumika lakini baadhi ya mifumo hiyo imekuwa haileti matokeo yanayokusudiwa katika utekelezaji wa majukumu na shughuli za serikali.

“ Kwahiyo ni lazima kila mmoja wetu atafakari kwa uhalisia ni kwa kiwango gani mifumo hii tuliyo nayo itakwenda kufanya kazi, kwa sababu kwa upande mmoja tumekuwa tukilalamika kushuka kwa mapato, ilihali tunayo mifumo”, aliongeza.

Alisema hali  hiyo inatokana na kutokuwepo umakini wa kusimamia mifumo hiyo hali iliyosababisha kutokuwepo ufanisi sehemu za kazi na wakati huo huo kushuka kwa mapato na kuwataka baada ya mafunzo kwenda kuisimamia mifumo hiyo kikamilifu ili iongeze mapato zaidi kwenye maeneo yao.

Alisema endapo wataitumia mifumo iliyopo serikalini katika kukusanya mapato watapata fedha nyingi sanjari na udhibiti wa mapato yake kwa lengo la kuleta ufanisi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye halmashauri na mikoa yao.

“ Unakuta mtu anakusanya mamilioni ya fedha, anakaa nayo mfukoni na baadaye mnaanza kukimbizana naye, lakini baada ya mafunzo haya muhimu natumaini hali hiyo haiwezi kutokea tena”, alifafanua, na kuongeza,

“ Myazingatie mafunzo haya na twende tukayatumie, tukiamini kwamba siku moja unaweza kuulizwa na Mwenyezi Mungu hata kama sisi tutakuwa hatupo duniani, kwa maana nyie ndio wasimamizi na watekelezaji wa shughuli za kiserikali”,

Alisema kutokana na changamoto hizo, mwezi Machi mwaka huu Ofisi ya Rais- Tamisemi, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Taasisi ya Touch Foundation na Mradi wa Ps3 walifanikiwa kutengeneza toleo jipya lilorahisishwa la WINS plus ambalo lilitumia taarifa kutoka mfumo wa DHIS 2 kwa ajili ya kukokotoa mahitaji ya watumishi na kupunguza gharama kwa ajili ya kutembelea vituo kwa ajili ya kukusanya takwimu za watumishio, ambapo mwezi April mwaka huu wadau hao walifanikiwa kutumia mfumo wa WISN plus POA iliyorahisishwa kuandaa taarifa za mahitaji ya watumishi kwa kuzingatia uzito wa kazi kwa halmashauri zote 185.

Katika utekelezaji wa ufanisi wa mfumo huo, alisema serikali inatarajia kuajiri katika sekta ya afya watumishi wapya 7,680, ambapo kati ya hao 6,180 ni wa Ofisi ya Rais- Tamisemi na 1,500 ni kutoka Wizara ya Afya na kwamba ni matarajio ya serikali kuwa halmashauri zitatumia ripoti za mfumo huo wa WINS plus POA iliyorahisishwa kusambaza watumishi wapya kwa kuzingatia uzito wa kazi na mahitaji kama yatakavyokuwa yameanishwa kwenye taarifa zao za ajira.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera(RMO)  Dk Marco Mbata licha ya kuishukuru PS3 kwa kuwekeza katika sekta ya afya na mifumo mbalimbali hapa nchini, ukiwemo mkoa wa Mbeya alipokuwa akifanya kazi kabla hajahamia mkoani Kagera, alisema mafunzo hayo yaliyotolewa kwa washiriki kutoka Mikoa ya Geita na Tabora yana manufaa makubwa kwa maendeleo ya nchi na watu wake endapo yatatekelezwa vyema na washiriki hao wa mafunzo.

Kwa upande wake Mratibu wa PS3 Mkoa wa Kagera Fabian Gapchojiga alisema kuwa pamoja na kwamba mradi wa PS3 ulilenga mikoa 13 nchini, umeamua kuendelea kuisaidia serikali kwa kuifikia mikoa ambayo haiku kwenye mradi kwa kusaidia kujenga mfumo wa WINS+ POA ambao badala ya kuisaidia mikoa 13 itatumiwa na mikoa yote nchini.

“ Ndiyo maana nasema leo tuko na mikoa ya Geita na Tabora ambayo haiku kwenye mradi wa PS3”, alisema.

Naye Mshauri wa Raslimali watu kutoka Mradi wa PS3 Geoffrey Lufumbi alisema lengo la mafunzo hayo ya siku mbili ni kuwajengea uwezo na uelewa watumishi hao juu ya utaratibu na matumizi ya upangaji watumishi kwa kutumia mfumo huo unaozingatia uzito wa kazi kwa ajili ya kuleta ufanisi kwenye maeneo yao ya kazi.

 Mfumo wa WISN plus POA hutumika kukokotoa mahitaji ya watumishi kwa kila kada katika vituo vya kutolea huduma kwa kuzingatia uzito wa kazi katika kituo husika.

Kwa sasa mfumo huu unatumika kwa ajili ya Vituo vya Afya na Zahanati tu, ukijumuisha kada mabalimbali zilizopo katika ngazi hizo za utoaji huduma ambazo ni Waganga, Waganga Wasaidizi , Tabibu , Tabibu wasaidizi , Maafisa wauguzi , Maafisa wauguzi wasaidizi na Wauguzi.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi