Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wateule kutoogopa kufanya maamuzi yenye nia njema kwa manufaa ya nchi.
Kauli hiyo ameitoa leo Ikulu jijini Dar es salaam wakati akihutubia mara baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni.
“Lakini niwaombe kwenye nia safi na ya kujenga nchi yetu msiogope kuja na mawazo ya kubadilisha mwelekeo wa nchi, kwa sababu kila mabadiliko yana ugumu wake, hakuna mabadiliko rahisi, watu wamezoea kushoto ukiwaambia geuka kulia watalalamika”, alisema Mhe. Rais Samia.
Pia Mhe. Rais Samia alibainisha kuwa, ili Tanzania iendelee ni lazima kupanga na kufikiri “Na mie niwaombe msiende kuona uoga katika kufikiri wala kuja na mapendekezo ambayo nyie mnaona yanaweza kuiendesha Tanzania vizuri. Kwa sababu kwenu ni kuwaza na kutuletea kisha vyombo mbalimbali vitakaa na kufikiri”.
Akizungumzia kuhusu suala la fursa, Mhe. Rais Samia alisema kuwa wakati Taifa linaendelea kulumbana kuhusu uwekezaji wa Bandari ya Dar es salaam, nchi jirani wao wanaomba kupata fursa hiyo ya kupata uwekezaji katika bandari zao na hivyo ni vizuri kuona fursa zinavyoweza kuja na kuondoka kwa haraka iwapo hazijatumiwa.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango alimpongeza Mhe. Rais Samia kwa kuirejesha Tume ya Mipango na kuiweka chini ya Ofisi ya Rais kwa kuwa ni chombo muhimu na kuwa maendeleo endelevu ya Taifa yanatokana na mipango inayaandaliwa na Tume hiyo.
Akitaja kazi kubwa tatu za Tume hiyo, Mhe. Dkt. Mpango alisema “Kubainisha hali halisi ya maendeleo ya nchi pamoja na changamoto na fursa zinazoikabili nchi, kubainisha mwelekeo wa nchi kimkakati kwa kipindi cha muda mfupi, wakati na mrefu na kazi ya tatu ni kuongoza maandalizi ya Dira ya Taifa ya Mwaka 2050. Sasa hayo ni majukumu makubwa kwa hiyo ukaongoze ufanyaji wa hizo kazi kwa kushirikiana na Wizara zote, na kwa msisitizo ukashirikiane zaidi na sekta binafsi, Chama Tawala, Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Benki Kuu ya Tanzania na Wizara ya Fedha”.
Kufuatia kutungwa kwa Sheria ya Mipango ya Taifa ya Mwaka 2023, Mhe. Rais Samia alifanya uamuzi wa kuhamishia masuala ya uwekezaji Ofisi ya Rais, ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko madogo ya miundo ya Wizara na kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali.