Benki ya Dunia (WB) imeahidi kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi unaoendelea wa Reli ya Kisasa-SGR na ukarabati wa Reli ya Kati-MGR, kutokana na umuhimu wa miradi hiyo katika maendeleo na uchumi wa nchi.
Ahadi hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete, aliyeongoza ujumbe wa benki hiyo walipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa na Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Bw. Belete alisema kuwa Benki ya Dunia ni mdau mkubwa wa maendeleo ya Tanzania na kwamba imeamua kushiriki katika ujenzi wa miradi hiyo miwili ya reli pamoja na kwamba kipaumbele kikubwa cha nchi kwa sasa ni ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR.
Alibainisha kuwa timu ya wataalam kutoka Benki ya Dunia na Tanzania wakutane haraka kuchakata mahitaji ya miradi hiyo ili benki itoe fedha za kuiwezesha nchi kutimiza malengo yake ya kukamilisha miundombinu ya reli hizo muhimu ambazo kukamilika na kuboreshwa kwake, kutasisimua uchumi, kuimarisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo, ndani na nje ya nchi.
Akizungumza kwa niaba ya Mawaziri wa Ujenzi na Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliishukuru Benki ya Dunia kwa utayari wao wa kusaidia ujenzi wa SGR na Reli ya Kati kutokana na umuhimu wake kwa Taifa kiuchumi na kijamii.
Pamoja na kujadili kwa kina kuhusu mradi wa Reli ya Kisasa SGR, kikao hicho, kilijadili pia masuala ya upatikanaji wa fedha za dharura kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua na Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Jijini Dar es Salaam-DART.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Makatibu Wakuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maanry Mwamba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamisi Shaaban, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, anayesimamia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, Viongozi wa Juu wa TRC, TANROADS, TARURA na DART.