Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri wa Kilimo Asisitiza Serikali Haitamlipa Kangomba
Feb 20, 2019
Na Msemaji Mkuu

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua maghala yaliyohifadhi korosho katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Pwani Februari 19, 2019. 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Pwani

Sheria ya Korosho kifungu cha 12 hakimruhusu mtu yeyote kufanya kazi ya korosho pasina kutambulika, wakati kifungu cha 15 cha sheria hiyo katika kifungu kidogo cha nne kinawataka wahusika wote wa korosho wawe wamesajiliwa na kuwa na leseni ya biashara hiyo.
Bila kuwa na usajili huo kwa mfanyabiashara yeyote wa korosho ni kosa kisheria hivyo kwa atanayebainika anapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Serikali imetilia msisitizo maagizo iliyoyatoa hivi karibuni kuwa katika malipo ya wakulima wa korosho haitamlipa mfanyabiashara asiyetambulika kisheria (Kangomba).
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo  tarehe 19 Februari 2019 wakati akizungumza na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Pwani.
Mhe Hasunga amesema kuwa ni lazima sheria zifuatwe katika utekelezaji wa majukumu yote ikiwemo biashara ya zao la korosho ili kuwanusuru wakulima wanaotumia nguvu nyingi katika kilimo hicho huku wakipata matokeo duni kutokana na baadhi ya wafanyabiashara wanaowahujumu (Kangomba).

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Wilaya ya Kibiti mara baada ya kukagua maghala yaliyohifadhi korosho ya serikali wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Pwani Februari 19, 2019.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisalimiana na Afisa Kilimo wa Wilaya ya Mkuranga Bi Julitha Bulali alipotembelea Wilayani humo kwa ajili ya kukagua maghala yaliyohifadhi korosho wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Pwani Februari 19, 2019.

Ameongeza kuwa wahujumu katika biashara za mazao mbalimbali ya kilimo nchini katika kipindi kirefu wamekuwa wakiwanyanyasa wakulima kwa kuwanyonya katika bei jambo ambalo serikali imelibaini hivyo kuingilia kati.

Aliongeza kuwa sababu ya wakulima kuchelewa kulipwa fedha za korosho zao kutokana na uhakiki uliochukua muda mrefu umesababishwa na vyama vya Ushirika kutofanya kazi yao ipasavyo kwa kuwasajili na kuwatambua wakulima.
“Vyama vya ushirika ndivyo vinapaswa kuwajua na kuwatambua wakulima wake katika mazao yote yanayouzwa kupitia mfumo huo, vinginevyo kutofanya kazi kwa weledi kumetuchelewesha kwa kiasi kikubwa” Alikaririwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa
“Hata sheria yetu ya maghala haikufanya kazi vizuri, Vyama vya msingi havikutekeleza majukumu yake”
Mhe Hasunga amesema kuwa serikali haitawavumilia wote wanaofanya biashara hiyo kinyume na sheria badala yake watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ameanza ziara ya kikazi mkoani Pwani, Lindi na Mtwara ambapo katika ziara hiyo atafuatilia mwenendo wa malipo ya wakuli wa zao la korosho.
   

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi