Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Ummy Atoa Ufafanuzi Kliniki za Madaktari Bingwa Baada ya Saa za Kazi
Jul 13, 2023
Waziri Ummy Atoa Ufafanuzi Kliniki za Madaktari Bingwa Baada ya Saa za Kazi
Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza kuhusu utaratibu wa kutoa huduma za afya binafsi baada ya masaa ya kazi.
Na Englibert Kayombo - Wizara ya Afya

“Utaratibu wa kutoa huduma za afya binafsi baada ya masaa ya kazi sio jambo jipya”, amesema Waziri Ummy na kuongezea kuwa utaratibu huo umekuwa ukifanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Mifupa MOI na Taasisi ya Saratani Ocean Road.

Waziri Ummy amesema kuwa utaratibu huo unasimamiwa na miongozo mahususi iliyopitishwa na bodi za Hospitali husika.

“Muhimbili utaratibu huu wanauita "Intramural Private Practice at Muhimbili (IPPM)", Wizara inaona kwamba ni jambo lenye tija kushusha utaratibu huu kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa”, ameeleza Waziri Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amefafanua kuwa utaratibu huo utawezesha wananchi kuhudumiwa kwa haraka lakini kwa kulipia kwa ziada, kuwatuliza madaktari kwenye vituo vyao vya kazi pamoja na kuwapunguzia adha ya kukimbia kwenye vituo vingine vya kazi baada ya muda wa kazi.

“Zoezi hili haliendi kuathiri utoaji wa huduma za afya kwa wananchi badala yake linakwenda kuboresha upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi katika maeneo yao.

“Utaratibu huu unalenga kuhakikisha tunavutia Madaktari Bingwa kufanya kazi mikoani, tumetangaza nafasi za Madaktari Bingwa 35 mwezi Juni, 2023 wakaomba madaktari 15, 11 walikidhi vigezo, wakaripoti Madaktari Bingwa 6 tu”.

Waziri Ummy amesema ni wajibu wa Serikali kuweka mazingira ya kuvutia Madaktari Bingwa kufanya kazi katika hospitali za umma.

Amesema kuwa utaratibu huo utazinufaisha hospitali kwa kuongeza mapato kwa kuwa watu wanaofika kwenye kliniki binafsi watalipia kwa gharama ya juu tofauti na wale wa muda wa kazi za mwajiri.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi