Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Simbachawene: Kazi Ndio Heshima ya Mtu
Aug 29, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi wetu- Dodoma

Wakristo nchini wametakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo, kuchangia pato la Taifa na kutatua changamoto zilizo katika maeneo yao.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene wakati akizunguma katika sherehe ya kumuweka wakfu Askofu wa  tatu wa Kanisa  la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa, Rev. George Chiteto iliyofanyika Jijini Dodoma baada ya aliyekuwa Askofu wa kanisa hilo, Donald Mtetemela kumaliza muda wake .

Waziri Simbachawene alisema changamoto nyngi za kiuchumi katika jamii zitatatuliwa endapo wananchi watajituma kufanya kazi na kuwa ubunifu kwa kuanzisha miradi mbalimbali kama ambavyo maandiko matakatifu yanaagiza watu kufanya kazi.

“Lazima wakristo wa sasa tufanye kazi lazima tutatue changamoto kwenye maeneo yetu maana imeandikwa katika biblia asiyefanya kazi na asile kwahiyo, kufanya kazi ndio uhai wako, heshima yako na ukizalisha utaweza kuendesha maisha yako binfasi, utashiriki katika kazi ya Mungu na Taifa zima,” alisema Waziri Simbachawene.

Pia aliongeza kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini kwani zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo, kusimamia maadili na kupambana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya watu wasio na hofu ya Mungu.

“Licha ya mchango mkubwa wa kanisa hili kwa Serikali lakini kumekuwa na mmomonyoko wa maadili, magonjwa na majanga mbalimbali hivyo ni muhimu kushirikiana na Serikali ili kuokoa vijana na watoto wetu na ni matumaini yetu viongozi wa dini mkiendelea kusimama  imara  na kutoa huduma ya kiroho tutatatua changamoto hii,” alieleza.

Aidha, alibainisha kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea  kuchukua hatua za kisheria kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, ufisadi, utovu wa nidhamu kwa watumishi wa umma pamoja na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Mhashamu Dkt. Maimbo  Mndolwa aliipongeza Serikali kwa kuwa mstari wa mbele kuziunga mkono taasisi za dini  katika nyanja zote huku akimtaka Askofu Chiteto kufanya kazi kwa kumtegemea Mungu hatimaye kufikia malengo ya kanisa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule  alitoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kutumia fursa ya Serikali kushusha bei ya  mbolea kwa kujikita katika kilimo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi