Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Mhe. George Simbachawene ameitaka Taasisi ya UONGOZI (UONGOZI Institute) kufanya tafiti za kimkakati zitakazoweza kuibua masuala mbalimbali ya kiuongozi kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.
Waziri Simbachawene ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa kuzungumza na Watumishi kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema tafiti hizo zinatakiwa zilenge katika kuibua mijadala ambayo itachagiza dhana ya utawala bora kwa kujikita zaidi katika kuibua changamoto zinazosababishwa na viongozi wenyewe barani Afrika.
"Tunataka mje na tafiti zitakazosomwa duniani kote ambazo zitaleta ukombozi kwa wananchi wa bara la Afrika hususan katika masuala ya uongozi mfano kwenye suala la rushwa", amesema Mhe. Simbachawene.
Amefafanua kuwa, kwenye masuala ya uongozi bado kunahitajika tafiti nyingi ambazo zitatoa dira ya kuwaandaa viongozi vijana wenye mtazamo wa kimapinduzi. Katika hatua nyingine, Mhe. Simbachawene ameipongeza Taasisi hiyo kwa kazi kubwa inayofanya ya kuwaandaa viongozi wa ndani na nje ya nchi pamoja na kukutana na kuzungumza na viongozi mbalimbali.
"Ninajivunia kwa kazi zenu kwani huko nje taswira yenu ni kubwa mno na ya kimataifa kutokana na jitihada zenu mnazofanya za kuhakikisha Afrika inakuwa na viongozi wenye kuwahudumia wananchi", amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Mhe. Ridhiwan Kikwete ameihimiza Taasisi hiyo kuendelea kuandaa viongozi wa baadae watakaoweza kuendeleza mazuri yanayofanywa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi yake, amesema atatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa ikiwa ni pamoja na kutoa tafiti zitakazoleta matokeo chanya katika jamiii na taifa kwa ujumla.