Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa ameelekeza watendaji wa Sekta ya Ardhi nchini kuhakikisha ndani ya siku mia moja kuanzia Septemba 4, 2023 wanatatua migogoro ya ardhi kwa kadri ya uwezo wa nafasi zao.
Aidha, ametaka waliovamia maeneo ya wazi kuanza kuondoka mara moja huku akielekeza viongozi na watendaji wa Wizara ya Ardhi wenye mamlaka ya kusimamia sheria kuhakikisha ndani ya siku hizo mia moja maeneo hayo yanakuwa wazi.
Waziri Silaa ametoa kauli hiyo wakati akizumgumza na Menejiment ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mara baada ya kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake Dkt. Angeline Mabula tarehe 4 Septemba, 2023 katika ofisi za wizara hiyo eneo la Mtumba Dodoma.
"Nawaomba na kuwaelekeza watendaji wote ambao sheria imewapa mamlaka kwa kiasi chao cha kutatua migogoro ndani ya siku hizi mia moja atatue kwa kadri ya uwezo wake.
Waziri huyo wa Ardhi amewataka pia watendaji wa sekta ya ardhi kusimamia haki halali wakati wa kutekeleza majukumu yao bila kujali sura wala rangi huku akionya wanaotumia fedha kunyima haki za wengine.
Silaa alielezea pia suala la migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye maeneo mbalimbali na kubainisha kuwa, maelezo ya Rais Samia Suluhu Hassan katika utatuzi wa migogoro ya àrdhi katika maeneo wanayoishi wananchi ni lazima busara itumike.
"Mhe. Rais ameelekeza kuwa katika utatuzi wa migogoro ya ardhi, katika maeneo ambayo wananchi wanaishi busara itumike, kwa sababu wale ni watu na wakati mwingine maamuzi yakifanyika kuwaondosha athari inaweza kuwa kubwa kuliko faida, naomba hilo mlizingatie", alisema Silaa.
Akigeukia suala la ufanisi kazini, Silaa ametaka mabadiliko makubwa katika utendaji ili kuleta ufanisi wa kazi huku akiahidi kuwepo mifumo mizuri itakayohakikisha kazi wanazofanya watendaji zinapimika, kuelekezeka sambamba na kuifanya serikali kuweza kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.
Kuhusu mifumo ya Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), amesema amesikitika kuona watu wakielezea matumizi ya mifumo huku wananchi wakiendelea kwenda kwenye ofisi kuhitaji baadhi ya huduma za mifumo hiyo.
Pia alielezea suala la vituo vya mafuta na kubainisha kuwa ipo Kanuni ya Mwaka 2018 inayotaka kituo cha mafuta kiwe umbali wa mita za mraba 400 yaani mita 20 kwa 20 na kusema kuwa kuanzia tarehe 1 Septemba, 2023 wote walioomba kinyume na kanuni hiyo maombi yao yasimamishwe watakapokutana na kushauriana.
Awali wakati wa makabidhiano ya ofisi aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Dkt Angeline Mabula alisema, alipoingia na anapoicha wizara hiyo ana imani iko kwenye hali nzuri zaidi na ni imani yake Waziri Silaa atakuwa hana changamoto nyingi kama alivyozikuta wakati anakabidhiwa wizara.
“Nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa sekta ameisogeza vizuri na tunakwenda na tukumbuke ameifungua nchi, uwekezaji unakuja kwa kasi na sisi kama wizara ndiyo tunamiliki ardhi”, alisema Dkt. Mabula