Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameiagiza Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kuandaa taarifa kuhusu mgogoro wa Hakimiliki kwa kazi ya ubunifu wa michoro ya Tingatinga pamoja na kufuatilia Mtunzi na Mmiliki wa Wimbo wa "Malaika Nakupenda" kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kuwa Wimbo huo ni maarufu duniani na umekuwa ukirudiwa kuimbwa na watu mbalimbali.
Dkt. Ndumbaro ametoa agizo hilo Oktoba 11, 2023 jijini Dar es Salaam alipotembelea Ofisi ya COSOTA ikiwa ni ziara yake ya kwanza iliyolenga kufahamu majukumu ya Taasisi hiyo.
"Ubunifu ni kitu cha msingi sana katika maendeleo ya Taifa, hivyo usimamizi wa Hakimiliki kwa kazi hizi za ubunifu ni muhimu.Tanzania tumeridhia kuwa sehemu ya Soko Huru la Afrika (African Continental Free Trade Area -AfCFTA) na kazi za sanaa, uandishi na ubunifu wa watu wetu zitasambaa kwa kasi hivyo ni vyema tujipange katika kuzilinda kazi hizi, tuzisajili kwa wingi ili tusiibiwe," amesisitiza Dkt.Ndumbaro.
Ameeleza kuwa, baadhi ya kazi za Wasanii zimekuwa zikitumika katika mataifa mbalimbali duniani na kuleta mgogoro katika utambulisho wa Hakimiliki, pia mapato mengi ya Wabunifu wa kazi hizo yamekuwa yakipotea akibainisha kuwa kuna wadau kama Tingatinga ambao hawawezi kupambania haki yao wenyewe bila Serikali kuwasaidia.
Pia ameiagiza COSOTA ifanye Operesheni ya kupambana na Uharamia wa kazi za ubunifu katika maeneo mbalimbali nchini na pia itenge bajeti itakayowezesha Maafisa kuwafuata wadau ili kusajili kazi zao.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki nchini, Doreen Anthony Sinare amesema marekebisho yaliyofanyika katika Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki kuanzia mwaka 2019, 2022 na 2023 yameiwezesha Tanzania ianze kunufaika baada ya Bunge Kuridhia Mkataba wa Marrakesh ambapo Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) lilileta mradi wa kuandaa vitabu na tayari limeshatoa msaada wa vifaa kwa Chama cha Wasioona Tanzania vinavyoweza kutumika shuleni na vinatarajiwa kusambazwa katika Shule 7 nchini.
"COSOTA tumepokea maelekezo yote na tunaahidi kuyafanyia kazi kwa wakati," alisema Doreen.
Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Tanzania, Omary Mpondelwa ameishukuru COSOTA kwa ushirikiano inaowapatia huku akiwasilisha ombi kwa Waziri Dkt. Damas Ndumbaro aweze kuwasaidia wasioona na wenye uoni hafifu waweze kushiriki katika mashindano ya Michezo nchini ombi ambalo alilipokea na kuahidi kulifanyia kazi.