Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ameiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuanza mara moja zoezi la uwekaji anwani za makazi kwenye mtaa wa Jogoo uliopo katika Kata ya Mbezi Juu Jijini Dar es Salaam kufuatia kuwepo kwa mgogoro wa ardhi wa muda mrefu wa zaidi ya miaka 40 kwenye eneo hilo.
Eneo la Mtaa huo ambalo kabla ya Uhuru lilitengwa na Serikali kwa ajili ya kilimo cha mazao ya biashara, mwaka 1970 Rais Mstaafu wa Awamu ya Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alilirudisha kwa wananchi na baadae kutengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda, kazi ambao haijafanyika ipasavyo ambapo kwa zaidi ya miaka 40 mpaka sasa, wananchi wamejenga makazi ya kudumu.
Katika mkutano wa pamoja kati ya Waziri Nape, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete, na Wakazi wa Mtaa huo, Waziri Nape ametoa agizo hilo kati ya maagizo sita ya Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu ya kutaka maeneo hayo yaendelee kuwa makazi ya kudumu ya watu na kupewa anwani za makazi huku waliokabidhiwa maeneo hao kwa ajili ya shughuli za viwanda na hawakuyaendeleza maeneo hayo, wachukuliwe hatua za kisheria.
“Mheshimiwa Rais ameagiza waliopewa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na hawakuviendeleza wachukuliwe hatua za kisheria, pia ameagiza viwanja ambavyo havijarasimishwa virasimishwe haraka, na kuanzia sasa tutaweka anwani za makazi hapa jogoo”, amesema Waziri Nape.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete amesema mgogoro huo ulipitia katika wizara hiyo na kwamba maamuzi ya uwekaji wa anwani za makazi kwenye eneo hilo limefikiwa na pande zote.
“Niwahakikishieni ndugu zangu wa Jogoo, uamuzi huu umetoka kwa Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan, sisi wizara tunaufahamu, Rais wetu ni msikivu sana, niwahakikishieni kuwa hakuna mtu atakuja kuwasumbua” amesema Kikwete.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe amesema Wilaya hiyo imetekeleza zoezi la anwani za makazi na wamefanikiwa kwa asilimia 105 na kwamba zoezi hilo litaendelea kwa wakazi wa mtaa wa jogoo ambapo kulikuwa na changamoto ya utambuzi wa anwani za makazi.
Mkazi wa Mtaa huo, Bw. Peter Ogilo alimwambia Waziri Nape kuwa watu wengi wa eneo hilo wamezaliwa humo na hawana mahali pa kwenda kwa kuwa wanayatambua maeneo hayo tangu walipozaliwa na hivyo Serikali itambue kilio chao.
“Mheshimiwa Waziri mimi na watu wengi hapa tumezaliwa hapa, hatuna sehemu nyingine tunayoijua, hapa ni nyumbani kwetu, leo hii ni miaka 40 na siku 29 wazazi wetu walianza kuishi hapa tangu kipindi cha operesheni nguvu kazi, tulipokea agizo la Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kuwa eneo hili halitapewa anwani za makazi kwa sababu lina mgogoro, nikuhakikishie kuwa eneo hili halina mgogoro, tunaomba anwani za makazi” amesema Bw. Ogilo.
Eneo la Jogoo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 3,000, lina nyumba zaidi ya 8,000 na kaya 28,300 huku wakazi wakikadiriwa kuwa ni zaidi ya elfu 60.