Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amemuaga Balozi wa Pakistan hapa nchini, Mhe. Mohammad Saleem anayemaliza kipindi chake cha kuhudumu.
Katika tukio hilo ambalo limefanyika kwenye Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam, Waziri Mulamula amemshukuru Balozi Saleem kwa utumishi uliotukuka na kumpongeza kwa mafanikio makubwa aliyoyapata katika utendaji wake ambayo yataacha alama na kumbukumbu ya kudumu kwenye historia ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Pakistan.
“Wizara na Serikali kwa ujumla tunajivunia utendaji wako, katika kipindi chako ulichohudumu hapa nchini licha ya kudumisha na kukuza uhusiano baina yetu na Pakistan, umefanya kazi nzuri sana ya kuibua fursa na mikakati mbalimbali ambayo imeleta manufaa kwa wananchi wetu, kama vile fursa za nafasi za masomo, kuendeleza shughuli za uvuvi nchini na kukuza biashara baina ya Tanzania na Pakistan”, Alisema Waziri Mulamula.
Balozi Saleem kwa upande wake ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano mzuri iliompa katika kipindi chote alichokuwa nchini kutekeleza majukumu yake. Aidha, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya usimamizi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri inayoendelea kuifanya ya kuleta maendeleo nchini.
Waziri Mulamula amemuhakikishia Balozi Saleem kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Pakistan kwa manufaa ya maslahi mapana ya pande zote mbili.
Wakati huo huo, Waziri Mulamula amempokea na kufanya mazungumzo na Balozi wa Misri nchini Tanzania, Mhe. Mohamed Gaber katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam. Wawili hao wamejadili masuala mbalimbali yenye maslahi kwa pande zote mbili ikiwemo uwekezaji, biashara, elimu na mafunzo, ushirikiano katika sekta ya utamaduni na michezo na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali inayotekelezwa na Kampuni za Misri hapa nchini.
Aidha, wamekubaliana kuendelea kufuatilia utelezaji wa makubaliano na mikataba mbalimbali iliyosainiwa wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini Misri mwezi Novemba 2021.