Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewaagiza Wazalishaji wa Madini ya Chumvi nchini kuzalisha kwa wingi na kwa ubora ili kukidhi viwango vinavyohitajika katika soko la ndani na nje.
Amesema hayo, wakati akifunga Maonesho ya Kwanza ya Madini na Fursa za Uwekezaji mkoani Lindi Agosti 26, 2023 Wilayani Ruangwa ambayo yalihusisha zaidi ya washiriki 140 kutoka ndani na nje ya nchi.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema, lengo la maonesho hayo ni kutangaza fursa za Uwekezaji katika Sekta ya Madini zilizopo mkoani humo.
Aidha, ameitaka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuendelea kufanya tafiti mbalimbali za madini ili kugundua maeneo mapya ya uchimbaji Madini kwa lengo la kuongeza wigo na fursa za ajira kwa Watanzania.
Sambamba na hayo, Mhe. Majaliwa amesisitiza uongezaji thamani madini kufanyika nchini kwa lengo la kuzalisha bidhaa zenye ubora zinatokana na Madini na kuongeza ajira kwa Watanzania hivyo kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Pia, Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote nchini kuandaa mpango wa uchimbaji endelevu, salama na utunzaji wa mazingira.
Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete ameipongeza Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya Uwekezaji na kuwataka wananchi wa Mkoa wa Lindi hususan Wilaya ya Ruangwa kutunza rasilimali zilizopo Mkoani humo ikiwemo ardhi.
Pia, Dkt Kikwete ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi kuchangamkia fursa za Uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini Mkoani Lindi ili kushiriki kikamilifu katika Uchumi wa Madini.
Naye, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amemshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maonesho hayo Mkoani Lindi ambapo amesema Wizara ya Madini itaendelea kusikiliza maelekezo yanayotolewa na viongozi ili kuipeleka sekta madini mbele.
Dkt. Biteko amesema Sekta ya Madini inaongoza kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni kutokana na kuuza bidhaa za Madini.
Katika Maonesho hayo zaidi ya wadau 140 kutoka Serikalini na sekta binafsi walishiriki katika viwanja vya Kilimahewa Wilaya ya Ruangwa, Mkoani Lindi kuanzia Agosti 21 hadi 26, 2023.