Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewatoa hofu wakazi 1,000 wa Manispaa ya Songea wanaoidai fidia ya sh. bilioni 3.8 ya eneo lao ambalo limechukuliwa na kuwa eneo la kiuchumi mkoani Ruvuma (Ruvuma SEZ) kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Ametoa ahadi hiyo leo (Jumamosi, Desemba 23, 2017) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Mwengemshindo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Manispaa hiyo.
Amesema Serikali ya awamu ya tano inatambua kilio chao ambacho alisema ni cha muda mrefu na kwamba alishawahi kupata ombi maalum kutoka kwa mbunge wao wa zamani, Bw. Leonidas Gama ambaye sasa ni marehemu.
“Alipotoka kutibiwa India alikuaja ofisini kwangu na kunieleza kwamba ana mambo mawili ambayo nikifanya ziara mkoani Ruvuma anaomba niyatafutie ufumbuzi. La kwanza lililkuwa ni hili la fidia kwa wakazi wa Mwengemshindo na la pili lilikuwa ni la ujenzi wa kituo cha mabasi cha mabasi cha mjini Songea,” alisema.
“Leo nimefanya ziara maalum kwa ajili yenu kwa sababu serikali ya awamu ya tano iko kwa ajili yenu na hasa wananchi wanyonge. Na tatizo hili inalijua. Kabla sijafika hapa, nilipita kwenye eneo husika na afisa mipango miji akanionyesha ramani ya eneo lenu hili,” alisema.
Waziri Mkuu aliwaeleza wakazi hao kwamba eneo hilo limetengwa na Manispaa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ambapo wawekezaji watatu tayari wamekwishajitokeza na wanataka kujenga viwanda vitatu.
“Kutakuwa na kiwanda cha kusindika mahindi, kutengeneza pumba za kuku na ng’ombe na mbolea. Kiwanda cha pili kitakuwa ni cha kusindika kahawa na cha tatu kitakuwa ni cha kukamua mafuta ya mbegumbegu,” alisema na kuongeza kwamba reli ya kutoka Mtwara kwenda Mbaba Bay inatarajiwa kupita kwenye eneo hilo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu kuchelewa kwa amlipo yao, Waziri Mkuu alisema kwamba katia ya wawekezaji hao watatu aliyekwishalipa fidia ni mmoja tu, na kwamba kwa mujibu wa sheria ya uwekezaji, fidia inapaswa kulipwa na mnunuzi wa eneo husika.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alikiri kuwepo kwa mapungufu wakati wa ulipaji kwa sababu walifuata orodha ya majina (kialfabeti) badala ya kutoa malipo kwa wakazi wa eneo husika. “Sasa hivi mwekezaji anataka kuanza ujenzi, lakini ndani ya eneo lake kuna watu ambao bado hawajalipwa, kwa hiyo hawawezi kutoka hadi wale waliobakia nao walipwe. Serikali itawafuatilia hawa wawekezaji wengine ili nao walipe fedha zao haraka ili waliobakia waweze kulipwa,” alisema.
Jumla ya watu 2,179 walifanyiwa uthamini mwaka 2008 na gharama yao kubainika kuwa ni sh. 3,254,737,622. Kuanzia Juni 8-19, 2015, Serikali iliwalipa wakazi 1,179 sh. 1,920,242,121 ambapo kati ya hizo, sh. 1,210,078,261 zilikuwa ni malipo ya thamani ya mali za wananchi na sh. 710,163,860 zilikuwa ni riba kutokana na malipo hayo kuchelewa kufanyika.
Eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 2,033 (sawa na ekari 5,000) lilitwaliwa na Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Ruvuma na Manispaa ya Songea tangu mwaka 2007. Eneo hilo linajumuisha mitaa ya Luwawasi (Mkuzo), Mwengemshindo na Luhira.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amemuagiza Afisa Ardhi wa Manispaa ya Songea, Bw. Kundaeli Fanuel Ndemfoo afuatilie suala la Bibi Monica Joseph Miti na wanae ambao walidhulumiwa nyumba ya urithi na aliyekuwa mwanasheria wa manispaa hiyo.
Ametoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Mwengemshindo baada ya kupokea bango lililoandikwa na Bibi Miti kuomba arejeshewe umiliki wa nyumba ya marehemu muwewe.
Alipopewa nafasi ya kueleza tatizo lake, Bibi Miti ambaye alimtaja mwanasheria huyo kwa jina moja la Bw. Mwakasungura, alidai kuwa mwanasheria huyo alighushi hati ya nyumba, na kuwatoa ndani ya nyumba yeye na watoto wa marehemu.
Alipoulizwa na Waziri Mkuu aeleze alipo huyo mwanasheria wa manispaa, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Bibi Tina Sekambo alijibu kwamba alishahamishiwa wilaya ya Ukerewe.
Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea na Afisa Ardhi wa Manispaa wafuatilie suala hilo na wampe majibu mapema iwezekanavyo. Pia amemuomba Bibi Miti na wanawe wafike kuonana naye Januari 3, mwakani atakapokuwa Songea kwa mapumziko mafupi ya mwisho wa mwaka.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake ya siku moja mkoani Ruvuma.
Imetolewa na:
Ofisi ya Waziri Mkuu,
Jumamosi, Desemba 23, 2017.