Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka madereva wa Serikali kuwa mfano kwa kuzingatia sheria zote hasa zile za usalama barabarani.
Mhe. Majaliwa amesema kwamba kuwa dereva wa Serikali haimaanishi kuwa uko juu ya sheria bali kila dereva anatakiwa kuwa mfano wa kuzingatia sheria zote ili madereva wa vyombo visivyo vya Serikali kujifunza kutoka kwao.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Oktoba 24, 2023 alipofungua Kongamano la Chama cha Madereva wa Serikali, katika Ukumbi wa Hoteli ya Morena mkoani Morogoro ambalo limebeba kauli mbiu inayosema Dereva wa Serikali bila ajali inawezekana. Kazi Iendelee.
Akizungumzia kauli mbiu hiyo, Waziri Mkuu amesema ni kweli inawezekana kuendesha magari ya Serikali bila kusababisha ajali iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake na kuzingatia sheria zilizopo, hivyo amewasisitiza madereva hao wahakikishe wanafuata sheria.
“Ninawapongeza sana kwa kuwa kaulimbiu hii pia ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025, Ibara ya 105 (K) ambayo inailekeza Serikali kuliwezesha Jeshi la Polisi pamoja na mambo mengine kuendelea na jukumu la kudhibiti ajali za barabarani,” alisema Mhe. Majaliwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeshafanya jitihada kubwa katika kutatua kero za watumishi wa kada hiyo ya udereva na bado inaendelea kuzitatua kwa kushirikiana na Chama chao.
Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara zenye dhamana husika bila kuathiri shughuli na majukumu yake ya kila siku ya kiutumishi, imebadilisha muundo wa ajira na kuondoa kigezo cha cheti cha ufundi (trade test) katika kuwapandisha madaraja na ngazi za mshahara kwa mwaka wa fedha uliopita.
Waziri Mkuu amewahakikishia madereva hao kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi zinaendelea kutekeleza azma yake ya kulinda maslahi ya madereva wa Serikali pamoja na kuyafanyia kazi maombi na ushauri utakaotolewa.