Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Ataka Watumishi OWM Waongeze Kasi
May 29, 2019
Na Msemaji Mkuu

Wazri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu waongeze kasi ili utendaji kazi Serikalini uweze kufikia hatua nzuri.

“Ninawashukuru watumishi wote kwa ushirikiano mnaotupatia mimi pamoja na mawaziri wenzangu, makatibu wakuu wote watatu, wakurugenzi mbalimbali na wakuu wa vitengo. Tunatakiwa tuongeze kasi ili tufikie hatua nzuri ya utendaji kazi Serikalini,” alisema.

Alitoa kauli hiyo jana usiku (Jumanne, Mei 28, 2019) alipokutana na viongozi na watumishi wa ofisi yake na kufuturu nao pamoja kwenye makazi yake jijini Dodoma.

Alisema utendaji kazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu ni mgumu kwa sababu unahusika na usimamizi wa shughuli za Serikali nzima na watendaji wote wa Serikali. “Sekta yetu ni ngumu kwa sababu sisi ni wasimamizi wa Serikali na watendaji wote wa Serikali. Tuna wajibu wa kuwaunganisha watendaji wa wizara zote serikalini,” alisema.

“Sisi sote ni watumishi wa umma, kwa hiyo mchango wenu una maana kubwa na unachangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Serikali nzima. Ninawapongeza kwa utumishi mwema na wenye uadilifu,” alisema Waziri Mkuu.

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa kufuturu pamoja, Waziri Mkuu alisema mwezi wa Ramadhan ni muhimu kwa Waislamu wote kwa sababu ni kipindi ambacho wanakamilisha nguzo kuu muhimu ya uislamu.

“Tukio la Ramadhan linatoa ujumbe mzito kwetu, ni wakati ambao tunatubu kwa maovu tuliyoyatenda. Wakati huu, inasisitizwa tuweze kushikamana, tujenge tabia ya umoja na pia tuweze kuvumiliana,” alisisitiza.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi hao, Waziri wa Nchi (OWM-SBAU), Bi. Jenista Mhagama alisema uamuzi wake wa kuwaalika watumishi na kufuturu nao ni dalili njema kuwa anathamini kazi zinazofanywa na watumishi walio chini yake.

“Ni viongozi wachache sana wanaowakumbuka watumishi walio chini yao. Tunakushukuru kwa kututhamini na tunaahidi kukupa ushirikiano wa dhati unaoenda sambamba na utendaji kazi uliotukuka,” alisema.

Akitoa shukrani kwa mwaliko huo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Waziri Mkuu na Bunge, Bibi Maimuna Tarishi alisema anatoa shukrani kwa niaba ya watumishi wote na kuahidi kufanya kazi kwa bidii.

“Tunaahidi kuongeza juhudi zaidi kwenye kazi zetu ili tuweze kuwa watu wa kupigiwa mfano na wengine,” alisema.

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

S. L. P. 980,

41193 – DODOMA.        

JUMATANO, MEI 29, 2019.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi