Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Ataka Mapitio ya Sera ya NGOs
Oct 04, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na WMJJWM Dodoma 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuanza mapito ya Sera ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001 ili iendane na mabadiliko ya Sheria ya NGOs ili kutoa fursa ya maboresho kwa Sheria, Kanuni na Miongozo inayosimamia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Oktoba 04, 2022 wakati akifunga Jukwaaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali jijini Dodoma na kuyataka Mashirika hayo kujikita katika kutoa huduma kwa jamii hasa iliyo vijijini ili wawafikie wananchi wengi zaidi ambao wanapatikana katika maeneo hayo.

Ameongeza kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanatakiwa kuboresha Mawasiliano na Mamlaka za Serikali za Mitaa maeneo walipo, kutoa taarifa sahihi ya shughuli wanazozifanya ili kuimarisha dhana ya uwazi na uwajibikaji na amezitaka Wizara, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa zihakikishe NGOs zinafanya kazi kulingana na usajili, malengo na vipaumbele vya Taifa 

 "NGOs zijielekeze kufanya kazi maeneo yenye uhitaji hususani vijijini badala ya kujitikita maeneo ya miji pekee na "NGOs ziendelee kubuni miradi endelevu ili ziweze kujiendesha, kupunguza na kuondoa kabisa utegemezi kwenye maeneo yanayotegemea fedha za nje", alisema Mhe. Majaliwa

"Wizara na Mamlaka za Serikali za Mitaa zifuatilie utekelezaji wa miradi na fedha zinazopatikana na kujiridhisha kwamba zinanufaisha wananchi na walengwa." alisema Mhe. Majaliwa

Pia, ameitaka Wizara kuanzisha Kitengo Maalum cha kufuatilia fedha za miradi zinazoletwa katika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuweza kujua fedha hizo zinatekeleza vipi miradi hiyo kwa manufaa ya jamii ili fedha hizo zitumike kama zilivyokusudiwa kusaida katika miradi mbalimbali nchini.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Mashirika hayo katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa jamii na ameyaomba Mashirika hayo kuanzisha ofisi zao katika Makao Makuu ya Nchi Dodoma ili kurahisisha utendaji kazi katika ya Serikali na Mashirika hayo.

Amezitaka Wizara za Kisekta ambazo hazijaanzisha Madawati ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuyaanzisha ili yaweze kusaidia Uratibu wa NGOs zinazofanywa kazi katika Sekta mbalimbali nchini ili ziweze kutekeleza miradi na kutoa huduma kwa jamii.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi