Taarifa kwa Umma
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea na kufanya ukaguzi katika eneo la mradi wa ujenzi wa gati kwenye Manispaa ya Lindi na kusema kwamba ameridhishwa na utekelezaji wake.
Pia amewaagiza viongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoa wa Lindi kujenga eneo la kupumzikia abiria kwenye maegesho ya kivuko katika maeneo ya Lindi na Kitunda ili wananchi wa maeneo ya Lindi na Kitunda waanze kupata huduma ya kivuko.
Waziri Mkuu alitembelea mradi huo jana (Ijumaa, Julai 14, 2017) wakati alipotembelea eneo hilo kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa gati hilo, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Lindi.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuondoa kero ya usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo, hivyo ujenzi wa gati hilo uende kwa kasi huku ukizingatia matakwa ya kiufundi na ubora wa hali ya juu.
“Jengeni sehemu ya kupumzikia abiria katika pande zote mbili, upande wa Lindi na wa Kitunda. Mbali na abiria kupata eneo la kupumzikia pia itarahisisha hata ukataji wa tiketi jambo litakawarahisishia ukusanyaji wa mapato.”
Pia Waziri Mkuu aliwaomba wananchi waendelee kuiamini na kushirikiana na Serikali katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kwamba ahadi zote zilizoahidiwa katika Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zitatekelezwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi kuyafanyia maboresho maeneo ya pwani na kuwa ya kisasa kwa kuondoa majengo yote chakavu ili wananchi waweze kuyatumia kwa ajili ya kupumzikia.
Alisema ni vema kwa manispaa hiyo kuainisha majengo yote ya zamani yaliyoko katika upande wa pwani yanayotakiwa kuhifadhiwa kwa ajili ya makumbusho ili yaweze kukarabatiwa na yaliyosalia yaondolewe.
Pia Waziri Mkuu alitembelea chuo cha Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoa wa Lindi na kusema kwamba ameridhishwa na utoaji wa elimu chuoni hapo na kuwaagiza viongozi waanzishe mafunzo ya mafuta na gesi ili vijana waweze kupata ujuzi na kuajiriwa kwenye sekta hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JULAI 15, 2017