Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Amwakilisha Rais Magufuli Kwenye Futari Chato.
Jun 22, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu.

  • Ahimiza nyumba za ibada zisitumiwe vibaya    

      WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba waumini wa dini za Kiislamu na Kikristo nchini, wahakikishe nyumba zao za ibada hazitumiki kuleta migogoro.

Ametoa ombi hilo jana jioni wakati akizungumza na mamia ya waumini wa dini za Kikristo na Kiislamu pamoja na viongozi wa dini walioshiriki futari wilayani Chato, mkoani Geita.

Akizungumza na waumini hao kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu alisema kuwa Mheshimiwa Rais alipanga kufika Chato ili kushiriki futari ya pamoja lakini kutokana na kutingwa na majukumu mengine ya kitaifa akaona ni vema amtume yeye (Waziri Mkuu) ili amwakilishe.

“Mheshimiwa Rais aliishapanga kuja Chato kufuturu pamoja na wana-Chato lakini kadri siku zinavyozidi kwenda anajikuta anabanwa na majukumu mengi ikiwemo kukutana na wageni wa kimataifa, kwa hiyo akaona ni vema nije kumwakilisha katika shughuli hii,” alisema.

“Mheshimiwa Rais anawaombea heri katika siku zilizobakia za mfungo wa Ramadhan ili mmalize salama na Mungu akijalia muweze kusherehekea pamoja, na pia anawatakia heri wale watakaoendelea na sita tushawal.”

Akisisitiza kuhusu amani na utulivu nchini, Waziri Mkuu alisema: “Hatupendi kusikia kuwa msikiti fulani wamechapana viboko kwa sababu ya kugombea uongozi au kwenye kanisa fulani waumini wamepigana wakigombea mchungaji wao.”

“Tutumie nyumba zetu za ibada kudumisha amani na mshikamano wetu. Napenda niwahakikishie kuwa Serikali yenu chini ya Rais John Pombe Magufuli itaendelea kuheshimu dini zote.”

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakumbusha waumini hao kwamba mwezi mtukufu wa Ramadhan ni wa toba kwa kila muumini. “Huu mwezi mafundisho yake yanasisitiza amani, uvumilivu na kusameheana. Nipende kuwasihi kwamba tuendelee kudumisha utulivu tulionao,” aliongeza.

“Nipende kusisitiza kwenu wana-Geita na wana-Chato kwamba jukumu kubwa mlilonalo ni kuendelea kumuombea Mheshimiwa Rais ili Mwenyezi Mungu amjalie afya njema, busara na uongozi wa kimungu katika maamuzi yake. Niwasihi ndugu zangu Waislamu na Wakristo, tuendelee kuwaombea viongozi wote wa kitaifa kila siku ili wafanye kazi kwa kuongozwa na Mungu,” alisema.

Awali, akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, Katibu wa BAKWATA Wilaya ya Chato, Sheikh Ally Moto alisema wanamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapa fursa ya kuweza kushiriki futari pamoja na watoto yatima na wajane.

Alisema wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano na ili kudumisha amani wilayani humo, waumini wa Kiislamu na Kikisto wameunda Kamati ya Amani ya wilaya hiyo inayojulikana kama Interfaith Committee.

Naye Mbunge wa Chato ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani alisema anamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuandaa futari hiyo ambayo imejumuisha wana Chato kutoka pembe nne za wilaya hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Geita, Askofu Mussa Magwesera wa Kanisa la African Inland Church (AIC), Dayosisi ya Geita alitoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais Magufuli na kuwapongeza viongozi wakuu wa kitaifa kutokana na utendaji wao unaogusa mioyo ya Watanzania.

“Ninyi wote watatu ni viongozi ambao Mungu amewaweka kuongoza nchi yetu. Katika miezi hii 18, mmefanya mambo makubwa, ni imani yetu kuwa ataendelea kuwaongoza katika utendaji kazi wenu,” alisema.

Akitoa shukrani, Sheikh wa Mkoa wa Geita, Sheikh Yusuph Kabaju ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa huo, alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapa fursa wana-Geita kujumuika pamoja katika futari hiyo na kuahidi kudumisha amani ya Tanzania.

“Tunakushukuru kwa kutuunganisha wana Geita katika futari hii japo umeamua kufanyia ibada hii hapa Chato. Maneno ya Quran tukufu yanasema malipo ya waliofunga anayapata pia yule aliyefuturisha waliofunga,” alisema.

Sheikh Kabaju pia alisoma dua ya kumuombea Mheshimiwa Rais Magufuli pamoja na viongozi wa kitaifa. Pia aliombea amani kwa ajili ya Taifa la Tanzania.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi