Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Akutana na Wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania Nchini Italia
Oct 17, 2023
Waziri Mkuu Akutana na Wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania Nchini Italia
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, wakati alipotembelea ubalozi huo, Roma, Italia Oktoba 17, 2023. Mheshimiwa Majaliwa alimuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani linalofanyika Makao Makuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) kuanzia Oktoba 16, 2023 hadi Oktoba 20, 2023.
Na Ofisi ya Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na watumishi wa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, ambapo pamoja na mambo mengine amewataka waendelee kuimarisha mahusiano ya kihistoria yaliyopo kati ya Tanzania na Italia.

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema nchi inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo, elimu, mifugo, afya hivyo wao waendelee kufanya kazi kwa bidii, weledi pamoja na kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini ili Taifa linufaike na uwepo wao nchini Italia.

 

Ameyasema hayo jana (Jumanne, Oktoba 17, 2023) wakati akizungumza na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia alipotembelea ofisi hizo zilizopo jijini Rome. Waziri Mkuu yuko nchini Italia akimuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan. Katika Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023.

 

“Nchi ipo salama, uchumi unaendelea kukua na lugha yetu kwa sasa ni maendeleo ya nchi na Serikali inaendelea kuimarisha sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo ambayo inawanufaisha Watanzania wengi na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza watendaji wawe wabunifu katika kuboresha sekta hiyo, hivyo endeleeni kufanya kazi mkiwa na amani.”

 

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wafanyakazi hao waendelee kuwatambua na kuwaunganisha Watanzania wote waishio nchini Italia pamoja na sehemu nyingine ambazo ubalozi huo unazihudumia. Pia amewataka watumishi hao waendelee kufundisha lugha ya Kiswahili kupitia darasa walilolianzisha kwani ni fursa muhimu katika kulitangaza Taifa na utamaduni wetu.

 

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo amemshukuru Mheshimiwa Majaliwa kwa kufanya ziara katika ofisi hizo za Ubalozi wa Tanzania nchini Italia na kwamba wamepokea maelekezo na ushauri alioutoa na wataufanyia kazi kwa maendeleo ya Taifa.

 

Tanzania na Italia zina ushirikiano wa kimaendeleo tangu kuanzishwa uhusiano rasmi wa kidiplomasia, ambapo Tanzania ilifungua Ubalozi wake mjini Roma mwaka 1972 na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania ulifunguliwa rasmi mwaka 1961.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi