Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Akutana na Balozi wa Umoja wa Ulaya na wa Jamhuri ya Korea
Feb 18, 2025
Waziri Mkuu Akutana na Balozi wa Umoja wa Ulaya na wa Jamhuri ya Korea
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimaina na Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini, Mheshimiwa Christine Grau katika mazungumzo yaliyofanyika kwenye Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam, Februari 18, 2025. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Ushirikiano kutoka Umoja wa Ulaya ( Head of Cooperation from the EU Delegation), Marc Stalmsns.
Na Ofisi ya Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Februari 18, 2025 amefanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Christine Grau, Ofisini ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es salaam.

 

Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Tanzania itaendelea kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji na nchi za Umoja wa Ulaya.

 

“Inatia faraja sana kuona kuna ukuaji wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na nchi za Umoja wa Ulaya, Umoja wa Ulaya umewekeza takriban Euro bilioni tatu nchini, hii kwa kiasi kikubwa imechangia kutengeneza ajira na makusanyo ya kodi.”

 

Amesema kuwa Tanzania itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji ili kuzivutia sekta binafsi kushiriki katika shughuli za maendeleo.

 

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Tanzania inathamini msaada mkubwa ambao unatolewa na Umoja wa Ulaya katika kuchangia shughuli za maendeleo nchini.

 

 “Katika kipindi cha 2021-2027, Umoja wa Ulaya umetenga Euro milioni 703 ili kusaidia mipango mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania, tunakushukuru hasa kwa kujitolea kwenu kuimarisha ushirikiano huu ” 

 

Awali, Mheshimiwa Majaliwa alikutana na Balozi wa Jamhuri ya Korea, Ahn-Eun-Ju ambaye alimweleza kuwa Tanzania inajivunia ushirikiano na nchi hiyo kwenye sekta mbalimbali za maendeleo.

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa Jamhuri ya Korea Nchini, Mheshimiwa Ahn Enju katika mazungumzo yaliyofanyika kwenye Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam, Februari 18, 2025.

“Tanzania na Jamhuri ya Korea zina ushirikiano mkubwa wa kibiashara kwa miaka mingi, mnamo mwaka 2023, kiwango cha ufanyajibiashara kilifikia Dola milioni 672.7, ikilinganishwa na Dola milioni 280.4 mwaka 2022.”

 

“Tunatambua kuwa makampuni ya Jamhuri ya Korea yamewekeza katika sekta mbalimbali nchini Tanzania kama vile viwanda, usafirishaji na ujenzi, hivyo kuchangia maendeleo ya nchi zetu. Tunathamini uwekezaji huu.”

 

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa alimweleza balozi huyo kuwa aone namna ya kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupata nafasi za kazi nchini Korea hasa kwenye sekta ya uzalishaji. “Kwa upande wetu sisi tutahakikisha Watanzania wanakuwa na vigezo stahiki vinavyohitajika ili waweze kufanya kazi ”

 

Kwa upande wake Balozi Ju alimweleza Mheshimiwa Majaliwa kuwa katika kipindi chote atakachohudumu kama balozi nchini atahakikisha anasimamia na kuendeleza masuala ya uwekezaji kwa faida ya nchi zote mbili.

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi