Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ujenzi Flyover Wakamilika kwa Asilimia 98 - Waziri Mkuu
Aug 30, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Paschal Dotto

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli imekamilisha ujenzi wa daraja la juu flyover lililoko TAZARA Jijini Dar es Salaam kwa asilimia 98.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukaguzi wa mwisho wa daraja hilo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema  kazi ya ujenzi wa barabara hiyo ya juu imefikia pazuri na Serikali inaendelea kuimarisha na kukamilisha miradi mikubwa nchini kama sehemu ya kutekeleza ahadi za serikali kwa watanzania.

“Leo tumekuja kukagua hatua za mwisho za ujenzi wa barabara hii hapa makutano ya TAZARA, kwa maandalizi ya uzinduzi utakaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John pombe Magufuli wakati wowote mwezi wa kumi” alisema Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa katika ujenzi huo ni vitu vidogovidogo tu ambavyo bado havijakamilika ili kuwezesha watanzania kuanza kufaidi matunda ya Serikali yao, jambo ambalo ni la kujivunia.

Mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Japani umefikia asilimia 98, ambapo barabara na njia  zote zimekamilika, taa pamoja na miundombinu mingine iko tayari kilichobaki ni ujenzi wa kiwango cha juu pembeni mwa barabara hizo ili kuzuia udongo na mchanga kuingia katika barabara.

Aidha Waziri Mkuu aliongeza kuwa ujenzi huo utarahisisha maisha ya wakazi wa Dar es Salaam hasa wanaotoka maeneo ya Gongo la Mboto, Mbagala na Pugu kwenda katikati ya Jiji kwa kuepusha adha ya foleni eneo la TAZARA, pia abiria kutoka uwanja wa ndege kwenda katikati ya Jiji watarahisishiwa usafiri kutokana na kupungua kwa foleni.

“Abiria wanaotoka uwanja wa ndege kwenda katikati ya Jiji, sasa watakuwa wanapita moja kwa moja ukilinganisha na awali ambapo ilikuwa ukifika hapa TAZARA lazima usimame kwa muda usiopunga dakika 40 mpaka 50 kusubiri taa ziruhusu, sasa itakuwa ni kupita moja kwa moja na inaweza kuwa ndani ya dakika 10 tu,” Aliongeza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu katika ziara hiyo pia alitembelea eneo la Ubungo ambako alikagua  ujenzi wa Mradi mkubwa wa barabara kuu ya Dar es Salaam- Morogoro.

Akieleza mpango wa Serikali wa kukamilisha ahadi zake kwa wananchi Waziri Mkuu,  alisema kuwa Serikali imejipanga kuwa mpaka kufikia Juni, 2020 mradi wa Ubungo utakuwa umekamilika.

Aidha Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam,Paul Makonda  kutenga eneo maalum kwa ajili ya wafanyabiashara wadogowadogo maarufu kama wamachinga walioko Ubungo ambako ujenzi unaendelea, ili wasi athiri utekelezaji wa mradi huo.

Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya tano inaendelea na ujenzi wa Miradi mikubwa ya mabasi yaendayo kasi ambapo awamu ya pili itajengwa katika eneo la katikakati ya barabara za juu flyover kutoka katikati ya Jiji kuelekea Gongo la Mboto- Pugu, Awamu ya tatu kutoka Katikati ya Jiji kwenda Mbagala-Kongowe, pia ujenzi wa Flyover nyingine kwenye makutano ya barabara za Mwenge, Morocco na makutano ya barabara ya uwanja wa taifa.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi