Na: Mwandishi Wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiasa jamii nchini kujiepusha na migogoro kwa vile haina tija na badala yake idumishe amani, upendo na uadilifu ili kumuezi mwanasiasa mkongwe nchini, marehemu Alhaj Ali Mtopa.
Aliyasema hayo jana (Jumatano, Aprili 11, 2018) alipomuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli katika mazishi ya mwanasiasa huyo yaliyofanyika katika kijijini Nanjilinji wilayani Kilwa. Alhaji Mtopa alifariki Jumatatu Aprili 9 jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu alisema haitapendeza kusikia jamii, wanafamilia, watendaji au wanasiasa waliokuzwa au kufunzwa na marehemu Alhaj Mtopa wakifarakana kwa sababu yoyote ile kwani siku zote marehemu alikuwa kiongozi aliyejitahidi sana kuwawaunganisha watu na mpenda amani.
“Tumepoteza kiongozi maarufu mwenye historia pana, amekuwa mtumishi ndani chama (CCM) na Serikali kwa muda mrefu. Alikuwa kiongozi mwema muadilifu, mtiifu na mchapakazi kwa miaka mingi”.
“Marehemu Alhaj Mtopa hakua mbaguzi kwenye kuielimisha jamii namna ya kuendesha siasaza kistaarabu. Kifo chake kinatuacha na huzuni, kazi yetu kubwa ni kumuombea ili Mwenyezi Mungu aweze kuilaza roho yake mahali pema”. Alisistiza Mheshimiwa Majaliwa.
Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi wanafamilia kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na baba ambaye alikuwa nguzo ya familia na jamii. Hivyo aliwaomba kutoruhusu mgawanyiko wa aina yoyote baina yao.
“Katika kipindi hiki kigumu ambacho tumeondokewa na mzee wetu na mwalimu wetu wa siasa na uongozi wetu nawasihi sana wanafamilia kuwa watulivu kwani haitapendeza kusikia kuwa kuna mgogoro au mgawanyiko kati yenu”.
Alisema yeye binafsi amepata msaada mkubwa kutoka kwa maremu Alhaj Mtopa katika masuala ya siasa na kijamii kwa vile mara nyingi akiwa katika ziara zake mkoani Lindi na katika jimbo lake la Ruangwa aliambatana na marehemu na kwa pamoja walishirikiana kutatua kero na kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mbali na Waziri Mkuu viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo, ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, Mbunge wa Mtama, Napa Nnauye na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi.
Wengine ni Mke wa Rais wa Awamu ya Nne na Mbunge wa Kuteuliwa Mama Salma Kikwete, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia na Pamoja na Waziri wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mbunge wa Kilwa Kusini,Selemani Ally Bungara na Mbunge mstaafu wa Mtama, Benard Membe.