Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa leo Septemba 8, 2023 ameahirisha Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma kwa kutoa maelekezo nane kwa Waajiri, Wafanyakazi, Mfuko wa Fidia wa Wafanyakazi, Wafanyabiashara, Maafisa Masuuli, Watendaji wa Serikali pamoja na Watumishi wa Umma.
Mhe. Majaliwa amewataka waajiri kuchukua hatua za kuimarisha mifumo ya kuwalinda wafanyakazi wao dhidi ya vihatarishi vilivyomo katika maeneo yao ya kazi; Hatua hizo ni pamoja na kuwa na mwongozo wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi, kufanya tathmini ya vihatarishi mahali pa kazi, kuhakikisha wafanyakazi wao wanapimwa afya ili kubaini athari ya vihatarishi kwa mfanyakazi na kuhakikisha maeneo yao yanafanyiwa kaguzi za usalama na afya ili kuwalinda wafanyakazi na kulinda uwekezaji wao.
Aidha, ametoa wito kwa Watumishi wa OSHA kuwa waadilifu wanapoendesha mazoezi ya ukaguzi mahali pa kazi na kuchukua vipimo vya wafanyakazi.
“Wafanyakazi wahakikishe wanazingatia taratibu na miongozo ya kujilinda dhidi ya Vihatarishi vinavyoweza kusababisha ajali au magonjwa wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao, hii itasaidia kulinda afya na usalama wao pamoja na kumpunguzia mwajiri gharama za uendeshaji pale wanapougua au kupata ajali wakiwa kazini,” ameelekeza Waziri Mkuu.
Vilevile ametoa maelekezo kwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuongeza wigo wa kutoa elimu kwa wafanyakazi ili watambue huduma zinazotolewa na mfuko huo; Pia, Waajiri watumie ipasavyo mifumo ya TEHAMA kupata huduma, kujisajili na kuwasilisha kwa wakati michango katika mfuko huo.
Aidha, Mhe. Majaliwa amewasisitiza Wafanyabiashara na watoa huduma kutoa risiti halali kupitia mashine za kielektroniki (EFDs) wakati wa mauziano ya bidhaa au utoaji wa huduma kwa wateja. Kwa upande wa wateja, amewakumbusha kuwa ni wajibu wao kudai risiti yenye thamani halisi ya fedha walizotoa.
Sambamba na hayo, Waziri Mkuu ametoa maelekezo kwa Maafisa Masuuli kuimarisha
usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na kutekeleza kikamilifu Mpango wa Bajeti ya
Mwaka 2023/2024.
Aidha, amewaelekeza Watendaji wa Serikali, kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kufanya matumizi kwa kuzingatia maeneo ya vipaumbele vilivyoainishwa katika bajeti sambamba na kubuni vyanzo vipya vya mapato.
“Watumishi wa umma mtenge muda wa kwenda kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika maeneo yao; Wafuateni, wasikilizeni na kutatua kero zao ili wasipoteze muda mwingi kufuatilia lakini pia wasilazimike kwenda ngazi za juu au kusubiri ziara za viongozi wa kitaifa kwa masuala ambayo mngeweza kuyafanyia kazi,” ameagiza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ameagiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria dhidi ya watumishi wote wanaosababisha upotevu wa mapato ya Serikali, aidha, amewaelekeza Wakuu wa Mikoa yote kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuwabaini wabadhirifu hao, kuwachukulia hatua mara moja na kutoa taarifa kwa mamlaka.