Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wahitimu 521 wa mafunzo ya Kozi Na..01/2023 wakatumie vema ujuzi na maarifa waliyoyapata katika kudhibiti vitendo vya uhalifu hususan maeneo ya vipenyo, vituo na mipakani.
Ametoa wito huo leo Ijumaa (Septemba 29, 2023) alipofunga mafunzo hayo kwa Askari wa Uhamiaji katika Chuo cha Mafunzo ya Uhamiaji cha Raphael Kubaga, Wilayani Mkinga, katika Mkoa wa Tanga.
Waziri Mkuu amemshukuru Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza kwa vitendo mpango wake wa kuvijengea uwezo vyombo vya ulinzi na usalama nchini.
Mhe. Majaliwa pia amewataka wahitimu hao wakafanye kazi kwa uzalendo, weledi na kutanguliza kwanza maslahi ya Taifa katika kazi zao za kila siku. “Kila mmoja akazingatie maadili na miiko ya kazi na akawe mfano bora wa uadilifu katika kituo atakachopangiwa,” amesisitiza.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa Jeshi la Uhamiaji wawachukulie hatua kali za kisheria wahitimu ambao watabainika kuwa wanajihusisha na vitendo viovu ikiwemo rushwa, wizi wa maduhuli ya Serikali, ama kujiunga na mitandao ya uhalifu wa kiuhamiaji.
Mhe. Majaliwa amesema kutokana na kuongezeka kwa teknolojia za kisasa na makosa ya kiuhalifu hususan biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu na uhamiaji haramu, wahitimu hao wanapaswa kuhakikisha wanapata maarifa mapya mara kwa mara ili waweze kukabiliana na mabadiliko hayo ya kiteknolojia.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Meneja wa TARURA Mkoa wa Tanga ahakikishe kuwa hadi kufikia mahafali ya mwaka 2024 awe ameijenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka barabara kuu inayoingia chuoni hapo.
Kuhusu changamoto ya maji kwa chuo pamoja na wananchi wa vijiji jirani, Mhe.Majaliwa ameiagiza Mamlaka za maji za Mkoa wa Tanga zihakikishe taasisi hiyo inaunganishwa kwenye mtandao wa maji. “Lakini pia Katibu Mkuu upo hapa, ona namna ya kuwezesha chuo hiki fedha kwa ajili ya ujenzi wa tanki la kuhifadhi kama yalivyo mahitaji ya chuo.”
Mapema, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni alisema awali Jeshi la Uhamiaji halikuwa likitoa mafunzo kwa watumishi wake.
"Mwaka jana ndiyo tulitoa kundi la kwanza la wahitimu, tunamshukuru Mhe Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa shilingi bilioni 1.5 za kuendeleza majengo. Hatukuwa na ajira mpya katika idara ya uhamiaji, tunamshukuru kwa kuongeza ajira wakiwemo hawa 521 wanaohitimu leo," alisema.
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mkinga, Bw. Dunstan Kitandula alisema anashukuru Serikali kwa uwepo wa chuo hicho na kuongeza: "Tunaiomba Serikali iendelee kuboresha chuo hiki kwa sababu matamanio yetu ni kuona chuo kinasaidia Afrika Mashariki yote."
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala aliiomba Serikali isaidie kuboresha miundombinu ya chuo hicho ikiwemo barabara ya kuingia chuoni na uwanja wa gwaride. Pia aliomba wajengewe tanki la lita 250,000 ili kutatua shida ya maji chuoni hapo na kwenye vijiji vya jirani.