Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuchika Awataka Watumishi Madini Kuwa Wazalendo
May 29, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Nuru Mwasampeta, Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapteni Mstaafu George Mkuchika amewata Viongozi na Watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake kuwa wazalendo ili kuifanya Sekta ya Madini   kuifikisha  nchi  katika uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025.

Kapteni Mkuchika amesema Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2025 Ibara ya 35 ni kuifanya sekta ya madini kukua na kuongeza mchango wake kwenye pato la taifa.

Ameyasema hayo Mei 28, 2019 wakati akifungua mafunzo ya siku Nne ya Viongozi wa Wizara na Taasisi zake pamoja na Maafisa Madini Wakazi kutoka mikoa yote nchini inayofanyika katika Ukumbi wa St.Gasper, Jijini Dodoma.

Mkuchika ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais John Magufuli kwa kusimamia Ilani ya Chama Cha Mapunduzi na kutekeleza ahadi kwa kuchukua hatua mbalimbali katika kuboresha sekta ya madini.

Akielezea hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano amesema ni pamoja na kuanzishwa kwa wizara ya mahususi ya madini, kutunga Sheria Mpya ya Usimamizi wa Madini, Kuunda Tume ya Madini, Kusimamia mifumo na maboresho kadhaa  katika sekta ya madini na kukiri kuwa, hatua hizo zinaonesha  dhamira ya Serikali kuifanya sekta ya madini kuchangia zaidi pato la Taifa.

Aidha, amesisitiza kuwa, ili Serikali iweze kufikia malengo yake, kila mmoja anapaswa kutanguliza uzalendo mbele katika kudhibiti vitendo vya kuhujumu jitihada za serikali vya kupambana na wizi na ubadhirifu katika sekta ya madini na sekta nyingine.

Vilevile, amewataka viongozi hao kuielewa na kusimamia Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, Sheria ya Utumishi wa Umma, Kanuni pamoja na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali lengo likiwa ni kuleta ufanisi wa hali ya juu katika utendaji unaozingatia sifa, weledi na maadili.

Pia, Waziri Mkuchika amekiri kufurahishwa na ushiriki wa viongozi wa Makao Makuu ya Wizara na taasisi zake katika mafunzo hayo na kuwataka kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu mafunzo hayo ikiwemo kuuliza maswali ili kupata ufafanuzi na uelewa  ili yawezeshe kuleta tija kwa wizara na taasisi zake.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko amesema kuwa, mafunzo hayo yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi yanatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa kwa watumishi wa wizara kuwafanya watekeleze majukumu yao bila woga.

Aidha, amemweleza Waziri Mkuchika kuhusu changamoto ya upungufu wa watumishi katika Sekta hiyo hususan wa Tume ya Madini na hivyo kutumia fursa hiyo kuiomba Serikali kulegeza masharti kwa watumishi waliofanyiwa upekuzi ili waweze kuteuliwa katika nafasi za uongozi.

“Mhe. Waziri kwa upande wa Tume ya madini kuna uhitaji wa watumishi 220, wizara ina uhitaji wa watumishi 61 na kuna nafasi  5  kati ya 61 za uteuzi ambapo nafasi 56 zilizobaki ni ajira  mpya,” amesisitiza Biteko.

Aidha, Waziri Biteko amekiri kuwa changamoto hiyo imetokana na kugawanywa kwa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini na hivyo kupelekea sehemu kuwa ya watumishi kuhamishiwa Tume ya Madini

Kutokana na hali hiyo, wizara imeomba kupata kibali maalum cha kuajiri watumishi wapya hususan katika kada za uhandisi migodi, mafundi sanifu, wajiolojia na jimolojia.

 “Mhe. Waziri tuna kiu ya kufanya mabadiliko na ni kubwa sana. Unaowaona hapa mbele yako wana kiu kubwa ya kuitumikia nchi na watanzania. Tuachieni kazi moja ya kuwaletea pesa mtupe watumishi,”amesisitiza Waziri Biteko.

Awali, Mkurugenzi wa Elimu kwa Viongozi kutoka Taasisi ya Uongozi Kadari Sengo amesema baada ya kufanya tathmini ya maeneo mbalimbali ya wizara ilibainika kuwepo kwa changamoto  katika maeneo kadhaa hivyo kuwepo haja ya kutoa mafunzo hayo ili kuboresha utendaji katika Sekta ya madini na hivyo kuleta tija zaidi.

Ameongeza kwamba, Taasisi ya Uongozi ina dhamana ya kuwajengea uwezo wa kiuongozi na utawala watumishi wa umma.

Akielezea sifa za kiongozi, amesema kuwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi ya kimkakati kwa faida ya taasisi yake, kuwa na uwezo wa kusimamia Rasilimali Watu na rasilimali nyingine katika taasisi yake pamoja na  kuwa mwenye kujiamini kwa kila jambo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuchika ametoa zawadi na vyeti kwa Wafanyazi Bora waliochagulikuwa kutoka Idara na Vitengo vya Wizara akiwemo Mshindi wa Pili Kitaifa kutoka  Tume ya Madini Fadhili Kitivai ambaye amepatiwa zawadi ya Shilingi Milioni Tano.

Aidha, Watumishi Edson Nkongo kutoka Kitengo cha TEHAMA na Milka Digha kutoka Idara ya Sera na Mipango wamepatiwa zawadi ya shilingi Milioni Mbili kila mmoja ya ufanyakazi Bora wa Wizara.

Wafanyakazibora kutoka Idara na Vitengo waliozawadiwa shilingi milioni moja kila mmoja pamoja na vyeti ni pamoja na Damian Kaseko kutoka Idara ya Sheria, Kashinde  Hamisi kutoka Idara ya Madini, Grace Paul kutoka Idara ya Utawala na RasilimaliWatu, Asteria Muhozya kutoka Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Laina Kasiga kutoka Idara ya Fedha,  Restuta Mwigani Idara ya  Ununuzi, Bethsheba Wambura kutoka Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani na  Kassim Kilanda kutoka TEITI.

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi