Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkenda Azindua Timu Kufanya Utafiti wa Ufuatiliaji wa Wahitimu wa Mafunzo ya Ufundi Kutoka Vyuo vya VETA
Aug 16, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mathias Canal, WEST-Dodoma

Serikali imetangaza timu ya watu watano kwa ajili ya kufanya Utafiti wa ufuatiliaji wa wahitimu wa mafunzo ya ufundi kutoka vyuo vya VETA nchini.

Timu hiyo itaongozwa na Dkt. Hamisi H. Mwinyimvua ambaye ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) na wajumbe wanne ambao ni Prof. Deograsias P. Mushi Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Dkt. John Chegere Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), Dkt. Claude Maeda Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Dkt. Ibrahim Kadigi Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Akitangaza timu hiyo ya Wataalamu hao leo tarehe 16 Agosti 2022 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa tafiti hizo zitalenga Kutathmini athari chanya au hasi za muda mrefu za programu mbalimbali za elimu, Kuboresha mitaala na mazingira ya elimu na mafunzo, kujua vikwazo wanavyopambana navyo wahitimu wanapoenda kwenye soko la ajira ili kuboresha, na kujua kama elimu au ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira au mahali pa kazi unaendana na elimu au mafunzo yanayotolewa na vyuo husika. 

Amesema kuwa malengo hayo yanaonyesha kuwa tafiti za ufuatiliaji zinatoa taarifa muhimu kwa wadau wanaohusika na utoaji wa elimu na mafunzo – kuandaa Sera ya Elimu na Mafunzo, kuandaa Mitaala ya elimu na mafunzo; n.k. ili kuhakikisha wale wote wanaohitaji elimu na mafunzo au ujuzi wa aina fulani wanapata fursa hiyo.

Pia malengo hayo yanaonyesha ajira na uandaaji wa Sera za Ajira – kuandaa Sera na Miongozo ya Ajira ili kuhakikisha wataalamu wa aina mbalimbali wanaohitajika wanakuwepo ili kutoathiri uwekezaji na ukuaji wa uchumi pamoja na ufanyaji maamuzi ya kifamilia au binafsi kuhusu aina gani ya elimu au mafunzo ya ujuzi mtoto au mtu asomee ili kukubalika kwenye soko la ajira au kuanzisha biashara binafsi.

Waziri Mkenda amesema kuwa kwa sababu ya msukumo mkubwa uliowekwa kwenye ujuzi, wadau wote wa elimu nchini wanapewa fursa ili waweze kutoa ushirikiano kwa kutoa maoni yao ili kuboresha elimu ujuzi.

Amesema kuwa Utafiti wa Ufuatiliaji au tracer study ni utafiti unaofanywa kufuatilia masuala mbalimbali ya wahitimu wa mafunzo mbalimbali kwa kutumia dodoso maalumu la mahojiano (questionnaire) kutegemeana na malengo ya utafiti huo. 

Waziri Mkenda amesema kwa kuelewa kuwa wahitimu wa mafunzo ya VETA wameongezeka kutoka 179,930 mwaka 2016 hadi 295,446 mwaka 2020, na utafiti wa mwisho wa aina hii ulifanyika mwaka 2018 kwa waajiriwa wa 2010 – 2015, malengo ya Utafiti wa Ufuatiliaji unaofanywa na Timu hiyo itakuwa ni Kujua walipo na wanafanya shughuli gani wahitimu wa mafunzo ya VETA baada ya kuhitimu masomo yao (waliohitimu 2017 – 2021). 

Malengo mengine ni kulinganisha mahitaji ya soko la ajira na uzalishaji wa wahitimu wa VETA (demand vs supply of graduates in the labour market), Kujua kama ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira unaendana na ujuzi unaofundishwa na vyuo husika, na Kujua kama kuna waajiri wasioajiri wahitimu wa VETA na sababu zake.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt Fransis Michael amesema kuwa timu hiyo ina kazi kubwa kuhakikisha kuwa inapokea maoni kutoka maeneo mbalimbali ili kuakisi uwajibikaji na ufanisi wa elimu ujuzi.

Amesema kuwa lengo kubwa katika ukusanyaji huo wa maoni ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapomaliza elimu ujuzi waweze kuajirika kirahisi katika maeneo mbalimbali waliyosomea.

Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ambaye ni kiongozi wa timu hiyo Dkt. Hamisi H. Mwinyimvua amesema kuwa utafiti wa aina ya ufuatiliaji unaweza kufanyika kujua walipo wahitimu wa kada au ujuzi fulani  (graduates) au wahitimu kutoka chuo fulani (alumni). 

Dkt Mwinyimvua ameongeza kuwa lengo la ufuatiliaji linaweza kuwa kujua ajira/shughuli wanayofanya baada ya kuhitimu, jinsi wanavyotumia ujuzi walioupata na changamoto wanazopambana nazo. 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi