Na. Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa kufufuliwa kwa kiwanda sambamba na shamba la Miwa la Mbigiri litasaidia kuondoa uhaba wa sukari nchini kwa kuzingatia uwepo wa kiwanda hicho na shamba la miwa Mbigiri.
Ameyasema hayo mapema mwishoni mwa wiki hii walipokuwa katika ziara na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kujionea namna uboreshaji wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na Jeshi la Magereza unavyoendelea.
Alieleza kuwa, tayari hekari 300 zimeshapandwa miwa kati ya Hekari 1200 na hekari 700 zimeshalimwa ambapo hii itasaidia sana kuongeza uzalishaji wa sukari nchini tofauti na ilivyo sasa na kuwaomba Watanzania kuunga mkono jitihada za Mifuko ya Hifadhi ya PPF na NSSF ambao wamechangia asilimia hamsini kwa hamsini katika kuhakikisha kiwanda na shamba vinafikia malengo ya kuzalisha sukari kwa wingi nchini.
“Ninaipongeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF kwa kuona umuhimu wa kukiboresha kiwanda hiki ili kukidhi hitaji la nchi katika kutatua changamoto ya sukari nchini ambapo matarajio ni kuvuna miwa tani 500,000 na uzalishaji wa sukari utakuwa Tani 30,000”Alisisitiza Mhagama
Sambamba na hilo, Waziri Mhagama alifafanua kuwa uwepo wa viwanda hivi ni moja ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Miaka mitano unaoelekeza kuwa na uchumi wa viwanda.
“Kiwanda hiki kikianza kufanya kazi kitakuwa kimekidhi matakwa ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa ya miaka Mitano ambao unaeleza uchumi wetu wa viwanda uwe uchumi utakaotumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini na bidhaa zitakazo zalishwa ziwanufaishe Watanzania”Alisema Mhagama
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa alieleza kuwa Kiwanda hiki kikimalizika kitasaidia kuongeza uzalishaji wa sukari nchini na kupata masoko mpaka nchi za nje.
“Jambo hili likifanikiwa litaweza kutatua changamoto ya sukari hapa nchini basi sisi kama Kamati na kwa niaba ya wajumbe wenzangu tunaipongeza sana Serikali kwa hatua kubwa iliyofanya na hii itasaidia pia kujikwamua kiuchumi sisi kama Nchi ” alisisitiza Mtengerwa
Aidha Mkurugenzi Mkuu Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Prof. Godius Kahyarara alieleza kuwa lengo jingine la kukifufua kiwanda hicho ni pamoja na kukuza uchumi wananchi kwa kuuza sukari ndani na nje ya nchi.
“Tunatarajia kupata soko la ndani na nje hususani kuuza ukanda wa Afrika ya Kati hivyo sukari itakayozalishwa lazima iwe ya viwangi vya juu na mfano mzuri ni nchi ya Congo ambao wanazalisha tani elfu 70 ingawa hitaji lao kwa mwaka ni tani laki moja hii ni picha halisi la uwepo wa siko la sukari barani Afrika” Alieleza Prof.Kahyarara
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Stephen Kebwe alipongeza juhudi za Serikali kufufua kiwanda hicho cha Mbigiri na shamba la miwa ambapo vitaleta tija kwa jamii kwa ujumla na kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge kuona umuhimu wa kutembelea Kiwanda hicho na Shamba la Miwa.