Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Angeline Mabula ameshiriki Mkutano wa Pili wa Baraza la Mawaziri wa Kamisheni ya Bonde la Mto Songwe uliofanyika leo tarehe 13 Julai 2023 Jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wa siku moja unaoongozwa na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Awesu unahusisha viongozi na wataalamu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Malawi huku ujumbe wa Malawi ukioongozwa na Waziri wake wa Maji na Usafi wa Mazingira, Mhe. Abida Sidik Mia.
Mawaziri wengine wa Tanzania wanaoshiriki mkutano huo ni Mhe. Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Deogratius Ndejembi na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato.
Mkutano huo ni muendelezo wa vikao vya pamoja baina ya Serikali ya Tanzania na Malawi unaolenga kuimarisha usimamizi, uhifadhi, uendelezaji na matumizi endelevu ya rasilimali ya maji ya mto Songwe.
Tanzania na Malawi zilishiriki majadiliano ya pamoja yaliyofanyika mwaka 1976 kuhusu namna bora ya kutatua changamoto zinazosababishwa na Mto Songwe kwa madhumuni ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu.