Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Kijaji Akagua Mito Tegeta, Segerea
Oct 03, 2024
Waziri Kijaji Akagua Mito Tegeta, Segerea
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akikagua athari za kimazingira katika mto Segerea Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya tarehe 02 Oktoba, 2024 akiwa ameambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis na watendaji kutoka ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Na Robert Hokororo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameielekeza ofisi ya Bonde la Mto la Wami Ruvu kidakio cha Pwani kutoa vibali vya kusafisha mto Tegeta ili kulinda mazingira na kupunguza athari kwa watu na mali zao pamoja na miundombinu ya umma.

 

Ametoa maelekezo hayo alipotembelea mto Tegeta uliopo wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam tarehe 02 Oktoba, 2024 na kujionea hali halisi ya mto na uharibifu wa mazingira unaofanywa na wakazi wa maeneo hayo ikiwemo utupaji wa taka katika mto huo.

 

Mhe. Dkt. Kijaji amesema ni lazima kutafuta suluhisho la kunusuru kingo za mito na kupunguza athari za mafuriko na kusisitiza wale wote walioomba vibali wapewe kwa ajili ya kusafisha mto huo.

 

“Kipaumbele kiwe kwa vikundi vilivyosajiliwa vya maeneo haya na ndio maana Task Force (kikosi kazi) iko hapa, wafanye kwa haraka hadi Jumatatu Bonde watoe cheti," amesisitiza Mhe. Dkt. Kijaji.

Akijibu pendekezo la Mbunge wa Kawe, Mhe. Askofu Dkt. Josephat Gwajima la kutaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuitisha kikao cha wadau wote wanaochimba mchanga kwa ajili ya kuwaelimisha kuhusu utunzaji na usafishaji wa mito.

 

Hiyo, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameiagiza NEMC kwa kushirikiana na Kikosi Kazi kuandaa kikao hicho na kuwataka wenyeviti waliopo kwenye maeneo ya mito yote kufika na wawakilishi wa wananchi.

 

"Kwenye kikao hicho wenyeviti wote ambao wapo kwenye maeneo ya mito yote ishirini na kitu, waje na wawakilishi wa wananchi, ni vizuri pia kuja na wazee maarufu wanaojua historia ya maeneo husika ili tuongee lugha moja alafu tujadiliane kwa pamoja na mwongozo wetu uwe wa kijamii," amesisitiza.

Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Kemilembe Mutasa amesema taka zilizozagaa katika kiongo za mto zinaweza kusabisha madhara kwa wananchi.

 

Amesema kuwa kutupa taka kwenye eneo hilo si suluhisho la kuzuia maji yasiingie kwenye makazi ya watu bali uchafu ambao unaweza kuwa chanzo cha maradhi kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam.

 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEM,  Dkt. Immaculate Semesi amesema Baraza limepokea maelekezo ya Waziri na kwa kushirikiana na Mhe. Dkt. Gwajima pamoja na Kikosi kazi kikao cha wadau kitafanyika kwa ajili ya kupata mawazo yao na kuwaelimisha juu ya utunzaji na usafishaji wa mito hiyo.

 

Katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji aliyeambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis walitembelea Mto Segerea wilayani Ilala na kushuhudia kupanuka kwa kingo za mto huo na kuagiza usafishaji wa mto huo uanze mara moja ili kunusuru mazingira.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi