Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Kalemani Atoa Maagizo Mazito kwa Wakandarasi wa Umeme Vijijini
Jan 30, 2020
Na Msemaji Mkuu

Veronica Simba – Dodoma

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amekutana na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa kwanza na kuwapa maagizo mazito yanayolenga kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na viwango stahiki.

Mkutano huo uliofanyika, Januari 29, 2020 jijini Dodoma, ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara husika, Mhandisi Leonard Masanja, Bodi za Wakurugenzi na Menejimenti za Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na wasimamizi wa miradi husika kutoka wizarani, TANESCO na REA.

Moja ya maagizo aliyoyatoa Waziri ni kwa watendaji wakuu wa TANESCO na REA, kuziwajibisha kampuni tatu za wakandarasi ambazo utendaji kazi wake hadi sasa uko chini ya wastani kwa mujibu wa mikataba yao waliyosaini.

Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Urban & Rural Engineering Ltd ambayo utendaji wake katika wilaya za Kakonko na Kibondo mkoani Kigoma uko chini; JV Pomy Engineering Co. Ltd, Intercity Builders Ltd & Octopus Engineering Ltd (Kaliua, Tabora) pamoja na NIPO Group Ltd (Arusha).

Akifafanua, Waziri Kalemani alieleza kuwa, kampuni hizo tatu ni miongoni mwa kampuni saba ambazo zilibainika kufanya kazi chini ya kiwango na serikali ikatoa maelekezo kuwa zifanye marekebisho ya kuboresha utendaji wao ndani ya siku 14; hata hivyo ni kampuni nne tu kati ya hizo zilitimiza maelekezo husika.

“Nazidi kuelekeza; siku 14 mlizowapatia kwa barua zenu, kulingana na mkataba zikikamilika pasipo wao kurekebisha dosari hizo; chukueni hatua ya kufuta mikataba yao au kusitisha malipo yao pamoja na kutoa adhabu kulingana na mkataba ulivyo.”

Sambamba na maagizo ya kuziwajibisha kampuni hizo zenye utendaji duni, Waziri alizipongeza kampuni tano ambazo zimefanya vizuri kwa kuvuka kiwango cha mkataba hadi kufikia sasa.

Alisema, kwa mujibu wa mkataba, wakandarasi wote wanapaswa kukamilisha kazi ifikapo Juni mwaka huu lakini kampuni hizo zimevuka lengo kwa baadhi yake kukamilisha kazi kwa asilimia 100 hadi sasa, ikiwa ni miezi mitano kabla ya makubaliano na nyingine kufikia kiwango cha juu kabisa zikielekea kukamilisha kazi husika ndani ya muda mfupi ujao.

Kampuni hizo ni STEG International Services waliotekeleza mradi kwa asilimia 100 katika mikoa ya Songwe na Mbeya; Sengerema Engineering Group Ltd, mkoani Pwani (zaidi ya 99%); Derm Electrics Ltd, wilayani Handeni (99.2%); JV White City International Contractors and Guangdong Co. Ltd, wilayani Simiyu (96%) pamoja na State Grid Electrical & Technical Work Ltd, mkoani Lindi (97%).

Maagizo mengine aliyotoa Waziri ni kwa kila mkandarasi kuhakikisha anakamilisha kazi katika eneo lake ifikapo Aprili mwaka huu ili miezi miwili inayosalia (Mei na Juni) itumike kukamilisha marekebisho madogo madogo kabla ya kukabidhi rasmi ifikapo Juni, 2020.

Sanjari na hilo, aliwataka mameneja wa TANESCO wa wilaya na mikoa pamoja na wahandisi wanaosimamia miradi husika, kuhakikisha ifikapo Februari 15, mwaka huu pasiwepo na nguzo iliyosimikwa ikiwa haijafungwa nyaya za umeme, pasiwepo na eneo la mradi lisilo na transfoma na pasiwepo na eneo la mradi ambalo wateja hawajaunganishiwa umeme.

Aidha, Waziri aliagiza kila mkandarasi kukabidhi Mpango-Kazi wake kwa uongozi wa TANESCO na REA pamoja na Wakuu wa Wilaya ambao unaainisha majina ya vijiji vitakavyounganishiwa umeme kila wiki, kuanzia sasa hadi mwezi Aprili, ambao ndiyo wa mwisho kwa kila mmoja kuwa amekamilisha kazi.

“Taarifa hizo ziwafikie Wakuu wa Wilaya kabla ya Februari 5, mwaka huu. Niwaombe Wakuu wa Wilaya mfuatilie utekelezaji wa kazi husika kama ambavyo taarifa itakuwa imeainisha. Mkandarasi akishindwa kutekeleza kama alivyoainisha, chukueni hatua za kumkamata,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri alikemea tabia ya baadhi ya wakandarasi kutotekeleza kazi ipasavyo huku wakitoa kisingizio cha kutokuwa na vifaa. Alisema, wakandarasi wanapaswa kufahamu kuwa ununuzi wa vifaa ni jukumu lao maana wote wamelipwa na serikali ili kuwawezesha kutekeleza kazi zao ikiwemo hiyo ya ununuzi wa vifaa.

Vilevile, alitoa onyo kwa wapimaji wa miradi ya umeme (surveyors), hususan wale wanaokaa na fomu za wateja zaidi ya 10 kwa muda mrefu pasipo kwenda kutekeleza kazi husika, kuacha tabia hiyo mara moja vinginevyo watawajibishwa.

Waziri alitoa kalipio kwa mameneja wa TANESCO ambao kwa namna moja au nyingine wanaruhusu wananchi, hususan walioko maeneo ya visiwani kutozwa gharama kubwa za umeme na wazalishaji binafsi.

“Nimeambiwa baadhi ya visiwa ikiwemo Ukerewe, wananchi wanatozwa shilingi 2,500 kwa uniti moja ya umeme jambo ambalo siyo sawa maana bei iliyopitishwa na serikali kwa wananchi wote ambao matumizi yao hayazidi uniti 75 kwa mwezi ni shilingi 100 tu kwa kila uniti.”

Hata hivyo, Waziri alizipongeza Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wa TANESCO na REA kwa kufanya kazi nzuri hususan katika uunganishaji umeme katika maeneo mbalimbali nchini jambo ambalo liliungwa mkono na Naibu Waziri Mgalu wakati akifunga mkutano huo kwa niaba ya Waziri.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Waziri na Naibu wake walisema pamoja na uwepo wa changamoto kadhaa katika utekelezaji wa miradi ya umeme lakini kwa kiasi kikubwa watendaji husika wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana.

“Kimsingi tunawahitaji sana. Tunahitaji sana ushirikiano wenu na kujitoa kwenu ili kwa pamoja tufanikishe azma ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli ya nchi kuwa ya uchumi wa viwanda. Hili linawezekana kwa uwepo wa umeme wa uhakika na wenye gharama nafuu,” alisema Naibu Waziri.

Aidha, Naibu Waziri aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi ya REA akisema inapaswa kuigwa kutokana na utendaji kazi wake mahiri. “Bodi hii inatembelea maeneo mbalimbali ya mradi na kukutana na watendaji wa pande zote zinazohusika ambazo ni serikali, wakandarasi, wauzaji na wazalishaji wa vifaa  ili kujua changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Naye Kaimu Katibu Mkuu, Mhandisi Masanja aliwaasa wakandarasi husika kuhakikisha wanaongeza nguvu katika kukamilisha idadi ya wananchi wanaopaswa kuunganishiwa umeme kwa mujibu wa mikataba yao badala ya kuunganisha wananchi wachache na kuhamia kijiji kingine.

Kwa upande wao, watendaji wakuu kutoka TANESCO, REA na wakandarasi husika waliahidi kutekeleza maagizo yote waliyopewa na Waziri.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi