Na Reyson Mwase.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amekutana na Balozi wa Marekani Nchini, Dkt. Inmi Patterson na Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya kwenye Ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo jijini Dar es Salaam. Lengo la ziara ya mabalozi hao lilikuwa ni kufahamiana na kujadili namna ya kushirikiana katika miradi ya nishati nchini.
Akizungumza na Balozi wa Marekani Nchini Dkt. Inmi Patterson aliyeambatana na wawakilishi kutoka Shirika la Misaada la Marekani (USAID), Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC) na Mradi wa Power Africa uliopo chini ya MCC, Dkt. Kalemani alielezea mikakati ya Serikali ya kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana nchini kuwa ni pamoja na mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji wa Stieglers Gorge uliopo Rufiji mkoani Pwani, miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi ya Kinyerezi I, Kinyerezi II na Kinyerezi III na miradi ya nishati jadidifu kama vile upepo, jua na jotoardhi.
Dkt, Kalemani alisema Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeweka malengo ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 kiasi cha Megawati 5000 za umeme zinazalishwa na vijiji vyote nchini kupata nishati ya umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu.
Waziri Kalemani alitumia fursa hiyo kualika wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza kwenye sekta ya nishati ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa malengo ya Wizara ya kuhakikisha nishati inachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi.
Naye Balozi wa Marekani Nchini, Dkt. Inmi Patterson alipongeza mikakati mizuri ya Wizara katika kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana kwani pasipo umeme wa uhakika hakuna maendeleo yoyote.
Balozi Patterson alimhakikishia Waziri Kalemani kuwa nchi ya Marekani ipo tayari kushirikiana na nchi ya Tanzania hususan katika sekta ya nishati pamoja na sekta nyingine ili kuchochea kasi ya maendeleo nchini.
Wakati huo huo Waziri Kalemani akizungumza na Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya aliyemtembelea ofisini kwake mbali na kueleza mipango ya serikali katika kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana, aliomba nchi ya India kusaidia kupitia wataalam wake kushirikiana na wataalam wa Tanzania katika sekta ya nishati kutokana na kuwa na uzoefu mkubwa.
Aliendelea kusema kuwa Tanzania imekuwa na historia ndefu ya ushirikiano na kusisitiza kuwa umefika wakati wa kuboresha ushirikiano katika sekta nyeti ili uchumi wa nchi uweze kukua kwa kasi na Serikali kutimiza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025 yenye kufafanua kuwa nchi kuingia kwenye orodha ya nchi zenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kupitia uboreshaji wa huduma za jamii.