Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Kalemani afanya ziara katika kampuni ya TANELEC
Nov 23, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_23297" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye ofisi za kampuni ya kutengeneza transfoma za umeme ya TANELEC zilizopo jijini Arusha.[/caption]

Na Greyson Mwase, Arusha.

Aitaka TANESCO, REA kujipanga upya mahitaji ya  transfoma

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani tarehe 22 Novemba, 2017 alifanya  ziara katika kampuni ya kuzalisha transfoma za umeme ya TANELEC iliyopo jijini Arusha lengo likiwa ni kukagua shughuli za kampuni hiyo pamoja na kuangalia namna ya kutatua changamoto katika uzalishaji wa vifaa vya umeme nchini.

Akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt. Kalemani alisema mara baada ya kukagua shughuli za kampuni hiyo na kujiridhisha uwezo wa kampuni hiyo katika uzalishaji wa transfoma, ni wakati wa TANESCO na REA kujipanga upya katika mahitaji ya transfoma za kutosha na kuwasilisha mahitaji hayo kwa kampuni husika na kuongeza kasi ya miradi ya umeme nchini.

[caption id="attachment_23298" align="aligncenter" width="750"] Meneja Mkuu wa kampuni ya kutengeneza transfoma za umeme ya TANELEC, Zahir Saleh (kulia) akimwonesha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani moja ya mifuniko ya transfoma za umeme inayotengenezwa na kampuni hiyo.[/caption]

Alifafanua kuwa mapema Juni mwaka huu Serikali kupitia Wizara ya Nishati ilipiga marufuku uingizwaji wa nguzo za zege na transfoma ili kuepuka gharama kubwa na tatizo la kuchelewa kwa miradi.

Aliendelea kusema kuwa baada ya kutoa agizo hilo, ameamua kufanya ziara ili kubaini uwezo na mahitaji halisi ya  transfoma za umeme ambapo amebaini kuwa kampuni hiyo ina uwezo wa kuzalisha transfoma za umeme 10,000 wakati mahitaji halisi ya transfoma za umeme nchini yakiwa ni 6,500.

Alisema kutokana na uwezo mkubwa wa uzalishaji wa transfoma katika kampuni hiyo, ni wakati wa TANESCO na REA kukaa pamoja na kuainisha upya mahitaji  ya  transfoma za umeme nyingi zaidi ili kuendana na kasi ya  utekelezaji wa miradi ya umeme nchini.

Dkt. Kalemani mbali na TANESCO na REA, aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA Awamu ya  Tatu kuanza kuainisha mahitaji  yao mapema kwa kampuni hiyo ili pasiwepo na kikwazo cha utekelezaji wa miradi  ya umeme  vijijini.

[caption id="attachment_23299" align="aligncenter" width="750"] Msimamizi wa Idara ya Vyuma, Zakayo Mmbaga (kulia) akionesha jinsi mashine ya kukunja vyuma inavyofanya kazi kwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa pili kushoto)[/caption] [caption id="attachment_23300" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akipanda mti kama kumbukumbu ya ziara yake katika kampuni ya kutengeneza transfoma za umeme ya TANELEC, iliyopo jijini Arusha.[/caption]

“Nimeambiwa kuwa wakandarasi wachache wameagiza transfoma za umeme katika kampuni ya TANELEC, nitoe fursa hii kuwataka wakandarasi wote nchini kuagiza transfoma za umeme mara moja na kuanza utekelezaji wa miradi yao kwa kasi kubwa, pasiwepo na kisingizio cha kukosekana kwa transfoma za umeme,”alifafanua Dkt. Kalemani

Katika hatua nyingine Waziri Kalemani aliitaka kampuni ya TANELEC kuanza kulipa gawio lake kwa serikali kupitia Msajili wa Hazina kuanzia mwaka huu.

Alisema Serikali inamiliki asilimia 30 ambapo asilimia 20 zinamilikiwa na TANESCO na asilimia 10 kupitia Shirika la Maendeleo Nchini (NDC).

[caption id="attachment_23301" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( wa nne kutoka kulia waliokaa mbele) na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ( wa tatu kutoka kulia waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa  kampuni ya kutengeneza transfoma za umeme ya TANELEC, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mara baada ya kumalizika kwa ziara hiyo.[/caption]

Naye Meneja Mkuu wa Kampuni ya TANELEC, Zahir Saleh akielezea biashara ya transfoma za umeme katika kampuni hiyo alisema kampuni hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kusambaza  transfoma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kama  vile  Tanzania, Kenya na Uganda na nchi nyingine kama vile, Nigeria, Zimbabwe na Ethiopia.

Alifafanua kuwa, wateja wakubwa wa transfoma hizo ni pamoja na  wazalishaji wa umeme, wakandarasi wa miradi ya umeme na wateja binafsi na  kuongeza kuwa kampuni hiyo imejipanga zaidi kuhakikisha inaongeza kasi ya uzalishaji ili kukabiliana na mahitaji ya transfoma za umeme mara baada ya serikali kupiga marufuku uingizwaji wa transfoma za umeme kutoka nje ya nchi.

Alisema kuwa kampuni imepanga kuongeza ajira kutoka wafanyakazi 120 hadi 150 ili kuongeza kasi ya uzalishaji na usambazaji wa transfoma ndani na nje ya nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi