Na Rhoda James, DSM
Waziri wa Madini Angellah Kairuki mwishoni mwa wiki alikutana na Ujumbe wa Benki ya Dunia jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufahamiana na kuangalia hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa Miradi ya Madini inayotekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) unaofadhiliwa na Benki hiyo kwa kushirikiana na Serikali.
Pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho, Waziri Kairuki aliitaka Benki ya Dunia kuona namna ya kuwaendeleza Wataalam wa Sekta ya Madini ili kuwezesha uwepo wa Watalaam wa kutosha hususan katika masuala ya Uthaminishaji wa Madini ya Almasi, Tanzanite na madini mengine ya vito na pia masuala ya uongezaji thamani madini kwa ujumla.
Pia, alishauri umuhimu wa kuboreshwa kwa Mtandao wa Huduma za Leseni kwa Njia ya Mtandao (Online Mining Cadastre) ikiwa ni pamoja na kuunganisha mtandao huo na Mamlaka nyingine ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ili taarifa zote zinazohusu madini na mapato yatokanayo na madini ziweze kupatikana kupitia mtandao huo.
Vilevile, aliishauri Benki hiyo kuhusu uuzwaji wa Madini ya Almas kwa njia ya Mnada kama vile inavyofanyika kwa Madini ya Tanzanite, lengo likiwa ni kuwezesha Serikali kunufaika na madini hayo.
Aliongeza kuwa, baada ya Serikali ya Tanzania kupitisha Marekebisho ya Sheria ya Madini kupitia Sheria ijulikanayo kama (The written laws (Miscellaneous Amendements) Act, 2017), alisema kuwa, baadhi ya wawekezaji wameonesha wasiwasi kuhusu marekebisho hayo.
Hivyo, Waziri Kairuki amewataka wawekezaji kutokuwa na hofu kwani mabadiliko hayo yanalenga kuhakikisha kuwa Serikali inanufaika ipasavyo kutokana na rasilimali zake za madini. Aidha, alisema kwamba, nia ya Serikali kuhusu kuvutia wawekezaji iko palepale ilimradi wazingatie Sheria na taratibu.
Vilevile Waziri Kairuki alieleza kwamba, ni vema Benki ya Dunia ikaangalia namna bora ya kuhakikisha madini yote ya Tanzanite yanayouzwa nje ya nchi yanakuwa na Hati ya Uhalisia inayoonyesha chanzo cha madini hayo suala ambalo litawezesha Taifa kupata mapato stahiki kutokana na rasilimali hiyo.
Vievile, Waziri Kairuki alizungumzia suala la udhibiti wa utoroshaji madini na kusisitiza kuhusu kuwepo na namna bora ya kuzuia utoroshwaji wa madini ya Tanzanite ikiwemo kujulikana kwa idadi ya wachimbaji wadogo, wa kati, kiasi kinachopatikana na mahali madini hayo yanapouzwa.
Pia, Waziri Kairuki aliishukuru Benki ya Dunia kutokana na ushirikiano ambao umekuwepo baina ya Serikali kwa kipindi chote na kueleza kuwa, Serikali iko tayari kutekeleza miradi husika kikamilifu kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila aliiomba Benki ya Dunia kuleta Wataalam wa madini nchini ili waweze kutoa mafunzo katika vituo vya Madini nchini ikiwemo Chuo cha Madini Dodoma (MRI) na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) ili kuzalisha wataalam zaidi katika Sekta hiyo.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Tanzania Mhandisi Benjamin Mchwampaka alisema kuwa, tayari Serikali imefanya jitihada kadhaa za kuanzisha mfumo wa utoaji wa leseni kwa njia ya Mtandao. Aliongeza kuwa, kinachotakiwa sasa ni kuimarisha zaidi mfumo huo ili taarifa zote zinazohitajika na umma zinazohusu madini na mapato ya kodi na mrabaha ziweze kupatikana kwa urahisi na kwa uhakika.
Aidha, Kamishna Mchwampaka aliiomba Benki ya Dunia kukijengea uwezo zaidi Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kilichopo jijini Arusha ili kiweze kutoa mafunzo ya Utambuzi wa madini na Uongezaji thamani kwa viwango vya Kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bella Bird alisema zipo fursa nyingi kwa Sekta ya madini na hivyo kuiomba Wizara ya Madini kuhakikisha kuwa inatumia fedha zilizopo katika miradi husika na kwa wakati.
Naye, Mwakilishi Mwandamizi Mradi kutoka Benki ya Dunia ambaye pia ni Mtaalamu wa Madini kutoka Idara ya Nishati Endelevu nchini Merekani, Mamadou Barry, alisema kuwa, Wizara ya Madini ihakikishe kuwa inakamilisha ujenzi wa Kituo cha Madini kinachotarajiwa kujengwa eneo la Mererani kwa wakati ili kuwezesha minada ya madini na maonesho ya madini kufanyika kwenye kituo hicho, na hivyo kudhibiti utoroshwaji wa madini.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Masula ya Madini kutoka benki hiyo Sheila Khama aliishauri Serikali ya Tanzania kuona namna ya kushirikiana na nchi nyingine kama Afrika Kusini hususan kwenye Mikutano ya Uwekezaji madini ya Indaba ili kuendelea kuwavutia wawekezaji.
Aidha, alishauri Tanzania kujifunza kutoka nchi ya Ethiopia kuhusu namna ya kudhibiti Wachimbaji Wadogo wa madini ya dhahabu kwa kuwa, nchi hiyo unao mfumo bora Barani Afrika.
Pia, alisisitiza kuhusu umuhimu wa ushirikishwaji wa wanawake katika shughuli za madini nchini.