Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Jafo Awataka Wananchi Kulinda Miundombinu ya Miradi ya Mazingira
Jul 13, 2023
Waziri Jafo Awataka Wananchi Kulinda Miundombinu ya Miradi ya Mazingira
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na Watendaji Waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakati wa ziara yake ya kukagua Mradi wa Kuongeza Uhimili wa Mabadiliko ya Tabianchi katika Shehia ya kiongoni bonde la mto tovuni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar Julai 12, 2023. Katikati ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Dkt. Omar Shajak na kushoto ni Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Bi. Farhia Ali Mbarouk
Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewataka wananchi kuendelea kutunza miundombinu ya utekelezaji wa miradi ya mazingira iliyopo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuzuia uharibifu wa mazingira na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Jafo ameyasema hayo Julai 12, 2023 wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi tuta kupitia Mradi wa Kuongeza Uhimili wa Mabadiliko ya Tabianchi unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika Shehia ya kiongoni bonde la mto tovuni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar.

Kwa mujibu wa Jafo amesema, athari za mabadiliko ya tabianchi kwa sasa zimeanza kujionyesha katika baadhi ya maeneo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akitolea mfano Wilaya za Longido, Simanjiro na Kiteto ambapo dalili za wazi zimejionesha kwa mifugo kupoteza maisha kutokana na hali ya ukame.

“Kule Bara kwa sasa ukienda Wilaya za Longido, Simanjiro na Kiteto wafugaji wengi mifugo yao inakufa kwa sababu hakuna maji wala hakuna malisho na mito mingine imekauka maji na mfano mzuri ni Mto wa Ruaha Mkuu ambao ulipoteza uwezo wa kutiririsha maji kwa muda wa siku 100”, amesema Waziri Jafo.

Akifafanua zaidi, amesema kuwa kutokana na ukubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi pia baadhi ya maeneo ya Zanzibar ikiwemo kisiwa cha Pemba kumeanza kujionesha kwa dalili mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari hatua inayosabisha maji ya bahari kuingia katika maeneo ya wananchi.

Kutokana na changamoto hiyo, Waziri Jafo aliwataka wananchi wa Shehia ya Tovuni kulinda miundombinu ya ujenzi wa mradi unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman kutokana na eneo kuwa ni miongoni mwa maeneo yaliyopo katika hatari kubwa ya kumezwa na maji ya bahari.

“Maji haya ya bahari yakiingia katika mashamba yanasababisha mkulima aliyezoea kulima mazao ashindwe kuendelea na kilimo ikaonekana maeneo mengine ni lazima yawekwe matuta. Ofisi yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar tulifanya ziara ya miradi mbalimbali ya TASAF ili kujionea maeneo yote yanayohitaji ujenzi wa matuta ili kuzuia maji ya bahari kuingia katika mashamba”, amesema Dkt. Jafo.

Dkt. Jafo ameamua kutembelea mradi huo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kutokana na historia ya mradi huo kunaonesha mafanikio makubwa ambayo tayari yameanza kupatikana kupitia shughuli za kilimo zinazoendeshwa na wananchi.

Waziri Jafo amesema wanufaika wa mradi huo hawana budi kulinda miundombinu ya mradi kwani ni jambo la msingi katika kuhakikisha hakuna shughuli nyingine za kibinadamu zitazofanyika katika eneo hilo ikiwemo ufugaji kwa kuwa kusababisha kuporomoka kwa udongo uliopo katika tuta hilo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo akikagua mradi wa tuta katika Shehia kiongoni bonde la mto tovuni Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar aliyoifanya jana katika kukagua mradi wa kuongeza uhimili wa mabadiliko ya tabianchi unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar. Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Dkt. Omar Shajak.

“Tuzuie lango la maji, tufanye kazi vizuri ya kulinda maji ya bahari yasije kuchanganyika na maji ya eneo la mashamba haya na kusababisha mafuriko ya maji yatakayosabaisha tuta lililopo eneo hilo kuzidiwa na kusababisha kupasuka na kuleta hasara ambayo ingeweza kudhibitiwa”, amesema Dkt. Jafo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Dkt. Dkt Omar Shajak amemhakikishia Waziri Jafo kuwa maelekezo yote aliyoyatoa kwa Ofisi yake yatafanyiwa kazi ili kuhakikisha kuwa mradi huo unaleta tija na manufaa yaliyokusudiwa.

“Mhe. Waziri Jafo maelekezo yako tumeyasikia, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ndio msimamizi wa masuala ya mazingira hapa Zanzibar na pia katika ziara hii nimeongozana na Mkurugenzi wa Mazingira wa Ofisi hii, Bi. Farhia Ali Mbarouk ambaye pia amesikia maelekezo yako”, amesema Dkt. Shajak

Naye Afisa kutoka Wizara ya Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Bw. Mbaraka Mgau amesema ujenzi wa mradi huo ulianza Januari 2021 na kukamilika Juni 2021 ambapo jumla ya wakulima 271 wa Shehia ya kiongoni katika Bonde la Tovuni wananufaika kupitia mradi huo.

Akifafanua zaidi, Bw. Mgau amesema kabla ya kuanzishwa kwa mradi katika eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 6 mazingira ya eneo hilo la mashamba liliathirika kwa kiasi kikubwa na maji ya bahari ambayo yaliingia kwa kasi kubwa katika mashamba ya wananchi na hatua iliyorudisha nyuma juhudi za uzalishaji wa mazao ya wakulima ikiwemo kilimo cha mpunga.

“Huu ni msimu wa pili wa mavuno tangu mradi huu uanzishwe ambapo kiwango cha mavuno ya zao la mpunga kimeongezeka kutoka tani moja hadi tani moja na nusu. Tunashukuru Kamati iliyoundwa na wakulima wa Shehia hii kwa kutupatia ushirikiano mkubwa katika kutekeleza mradi”, amesema Mgau.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi