Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali imewekeza katika teknolojia ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi kupitia miradi ya mazingira inayotekelezwa nchini.
Dkt. Jafo amesema hayo alipochangia mjadala wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Septemba 08, 2023.
Ametoa wito kwa nchi zilizoendelea kuunga mkono juhudi hizo za Serikali kwa kufadhili miradi ya kilimo inayotekelezwa nchini ili pawepo na tija na uhakika wa chakula.
Kutokana na Makubaliano ya Paris kuhusu nchi zilizoendelea kuchangia fedha kwa mataifa yanayoendelea katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Waziri Jafo alipendekeza kupitia fedha hizo pia pawe na mafungu maalumu ya kuwezesha kilimo cha kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, Waziri Jafo alisema ili kukabiliana na changamoto ya ukame unaosababishwa na uhaba wa mvua katika baadhi ya maeneo Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya uchimbaji wa malambo 114 ya umwagiliaji.
“Tunafahamu sekta ya kilimo inaathirika sana kwa maana mvua hazitoshi hivyo miradi ya adaptation ni muhimu sana kama nchi hizo zikiwekeza katika teknolojia ya kilimo. Tuipongeze Serikali inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuja na Mradi wa BBT kwa vijana na tunaona umeanza kutimiza ndoto za vijana,” alisema.
Aidha, katika kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija pamoja na kuwepo kwa changamoto za kimazingira, Dkt. Jafo alisema Serikali inaimarisha uzalishaji wa nishati ikiwemo mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere na kusambaza umeme vijijini.
Alifanua kuwa hatua ya usambazaji nishati vijijini itasaidia kuwavutia wawezekaji kufungua viwanda vya uchakati wa mazao na hivyo kukuza uchumi kwa kuuza bidhaa zilizochakatwa badala ya mazao ghafi.
“Katika mkutano huu tumewataka wenzetu watimize wajibu wao kuchangia fedha za kusaidia nchi zinazoendelea katika miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi hasa kwenye smart agriculture kwani mvua hazitoshi kwa kilimo,” alisisitiza Waziri Jafo.