Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Jafo Apokea Taarifa ya Mto Msimbazi
Nov 01, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amepokea taarifa fupi ya usafishaji wa Mto Msimbazi kutokana na maelekezo aliyotoa hivi karibuni kwa Kikosi cha Kuratibu Usafishaji Mito na Mabonde Mkoa wa Dar es Salaam.

Taarifa hiyo imewasilishwa kwa Waziri Jafo ofisini kwake jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Kuratibu Usafishaji wa Mito na Mabonde Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Elizabeth Mshote.

Hivi karibuni alifanya ziara ya kikazi ya kukagua mto huo katika Kata ya Mogo Mtaa wa Kipawa baada ya kupokea malalamiko kuhusiana na athari za kimazingira zinazotokana na usafishaji wa mto huo.

Hata hivyo, wakati wa ziara hiyo baada ya kusikiliza maoni ya wananchi alipata maoni yanayokinzana ambapo wengine walidai shughuli za usafishaji mto huo zimeleta athari kwa mazingira na wengine wakidai zimeleta manufaa makubwa kwa jamii inayozunguka eneo hilo.

Itakumbukwa Februari 2021, Waziri Jafo alikutana na wadau wanaojishughulisha na uchimbaji mchanga katika mkoa huo kujadili changamoto za kimazingira zinazotokana na uchimbaji mchanga kiholela katika mito na mabonde ili kuweka utaratibu mzuri.

Kikao hicho kiliwezesha kuandaliwa Mwongozo wa usafishaji mito utakaotumika katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kuondoa mchanga, taka ngumu na tope ili kupunguza au kuondoa madhara ya mafuriko ambao ulitolewa kwa mujibu wa kifungu cha 57 (2) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi