Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa pongezi kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhifadhi mazingira.
Ametoa pongezi hizo aliposhiriki zoezi la upandaji miti katika viwanja vya Bombambili (EPZA) mkoani Geita ambapo amewashukuru kwa kutekeleza maagizo aliyoyatoa Agosti 12, 2022 wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa STAMICO.
Amesema kuwa shirika hilo lilikuja na Kampeni ya STAMICO na Mazingira at 50! kwa lengo la kuhakikisha pamoja na uendeshaji wa shughuli za uchimbaji wa madini kuhakikisha mazingira yanatunzwa kikamilifu.
“Mtakumbuka nilifanya ziara ya kushtukiza kutembelea eneo la Ipagala (Dodoma) kuona kama kweli mmetekeleza kwa vitendo maelekezo, nimekuta kweli mmetekeleza yote kwani niliona mmezungushia uzio na miti inaendelea vizuri sana,” amesema Dkt. Jafo.
Pia, ameshukuru STAMICO kwa kufanya kazi kwa pamoja na vikundi mbalimbali vikiwemo Kikundi cha Wanawake na Samia ambapo walipewa kazi ya kupanda na kutunza miti 560 eneo la EPZA ambayo inazidi kustawi.
Aidha, amewasifu kwa kuwapa uwakala wa kuuza nishati mbadala ya kupikia kwa Mkoa wa Geita, hatua itakayosaidia katika kuhifadhi mazingira kuepuka ukataji wa miti hovyo.
Katika zoezi hilo, jumla ya miti 340 ilipandwa pia na viongozi wengine akiwemo Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale, Grace Kingalame pamoja na viongozi wengine.